Vyama tawala nchini Ujerumani vimeonekana kukwama kuhusu mipango ya kuifanya chanjo ya virusi vya corona kuwa lazima vikisema inaweza kuchukua miezi kadhaa kwa wabunge kulijadili suala hilo lililo na utata bungeni.
Gazeti la kila siku la Tagesspiegel lilimnukuu Naibu kiongozi wa chama cha Social Democrats Dirk Wiese akisema bunge linapaswa kulenga kukamilisha mijadala yake juu ya chanjo wakati wa robo ya mwaka 2022.
Kwa upande wake kiongozi wa chama cha kijani bungeni Britta Hasselmann ameliambia shirika moja la habari kwamba mjadala wa kwanza juu ya hilo huenda ukafanyika mwishoni mwa mwezi Januari.
Hata hivyo uwepo wa vikao vichache vya bunge mwezi Februari kunamaanisha bunge halitoweza kupitisha mswada wowote hadi mwishoni mwa mwezi Machi na mchakato mzima huenda ukachukua muda hadi kupitishwa kwa msuada huo.
Miongoni mwa wale wanaopinga kulazimishwa kwa watu kuchomwa chanjo ni chama cha Free Democrats ambao ni sehemu ya serikali ya muungano na waziri wa fedha wa Ujerumani aliyeapa kutoanzisha mfumo huo wa chanjo ya lazima.