CCM Wasema Yanayofanywa Na Rais Samia Yanabaraka Zote Za Chama
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kazi zote zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia Watanzania ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na zina baraka za Chama hicho.
Kimesema Rais Samia amedhamiria kufungua uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja jambo ambalo limejidhihirisha kwa vitendo kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, katika dua maalumu ya kumuombea Rais Samia iliyofanyika Magomeni jijini Dar es Salaam.
"Rais Samia Suluhu Hassan ameimarisha na kuboresha mazingira ya biashara nchini hali iliyochochea biashara nyingi kurejea, ikiashiria kuwa hali ya biashara na uwekezaji nchini sasa ni rafiki na wezeshi, amesema.
Shaka amesema Rais Samia ameondoa urasimu katika usajili wa biashara na ameondoa ukusanyaji kodi kwa mabavu. Hali hii imewafanya Watanzania kuona fahari ya kulipa kodi kwa hiyari.
Ameongeza kuimarishwa kwa hali ya ufanyaji biashara kumechochea upatikanaji wa manufaa ikiwamo kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya Serikali.
Shaka ameeleza Rais Samia ameonyesha ubunifu na uwezo mkubwa wa kupanga vipaumbele na rasilimali za serikali, ikiwamo pia kuwa makini katika kuhakikisha kila shilingi inayokusanywa, inayozalishwa au inayopatikana inakwenda kuongeza thamani kwenye maendeleo ya nchi na maisha ya Watanzania.
"Ndio sababu tumejionea miradi mikubwa ya kimkakati ikiendelea, miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja ikiendelea, miradi ya maji nayo ikiendelea tena kwa kasi nzuri.
"Kazi zote hizi na nyinginezo anazofanya Rais Samia Suluhu Hassan ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, hivyo Chama kinaridhishwa na kasi yake na kinamuunga mkono kwa asilimia 100.
Amebainisha kutokana na kasi ya utendaji wa Rais Samia ni wazi kuwa amewanyima hoja wanaompinga, na sasa wameanza kuibua hoja zilizojaa mfumo dume na ubaguzi ambapo ametaka wapuuzwe kwani ni hatari kwa taifa.
"CCM ipo madhubuti, Tanzania ipo imara na salama kwenye mikono ya Rais Samia na niwapongeze Watanzania kila kunapoibuka jambo kubwa linalogusa maslahi ya taifa Watanzania wamekuwa wakiungana pamoja kulinda heshima na maslahi ya nchi kwanza, huu ndio utaifa na uzalendo wa kweli," alisema Shaka.
"Ni wazi Rais Samia ataendelea kufanya mema kwa Watanzania ambayo yatasaidia katika kuleta maendeleo endelevu katika kusukuma mbele mafanikio ya kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini," amefafanua
Kuhusu dua ya kumuombea Rais,Shaka amepongeza kufanyika kwa dua hiyo na kwamba anafanya kazi kubwa inayohitaji msaada wa maombia ili afanikiwe.
"Ninawashukuru sana viongozi wetu wa dini mliotuongozea dua na maombi kwa ajili ya Rais wa nchi yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Urais wa nchi ni jukumu kubwa na zito, linalolohitaji hekima, busara, afya njema, uadilifu, uzalendo na hofu ya Mungu ili kuweza kubeba matumaini na matarajio ya wananchi kwa kuwaongoza kwa haki na usawa pamoja na kuheshimu utawala wa sheria. Kwa hivyo dua na sala ni muhimu ili aweze kumaliza utumishi wake kwa mafanikio na salama, amesema.
Kwa upande wake Mbunge wa Kinondoni Abbas Tarimba amewaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa ni kiongozi aliyejipambanua kupigania maslahi ya wote
"Tumwombee Rais Samia, ni kiongizi wa mfano. Kitendo cha kwenda kukopa fedha nje na kuwaeleza Watanzania amekipa kiasi gani na zinatumikaje huku zikigawanywa na kuleta manufaa kwa nchi nzima, ni cha mfano na kinapaswa kupongezwa," amesema.
Dua hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kiislamu na Kikristo, iliandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Tawi la Magomeni Makuti kwa kushirikiana na umoja huo Wilaya ya Kinondoni.