Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameipongeza Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania kwa mafanikio makubwa ya kiuendeshaji na kufanikisha kuipatia Serikali zaidi ya shilingi bilioni 122 katika kipindi cha miaka miwili ikiwemo gawio pamoja na kodi nyingine.

Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo Jijini Dodoma alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Artel Tanzania aliyemaliza muda wake, Bw. George Mathen na Mkurugenzi Mtendaji Mpya wa kampuni hiyo, Bw. Dinesh Balsingh, waliomtembelea kwa ajili ya kuaga pamoja na kujitambulisha.

“Fedha hizo zimeiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya kijamii ambayo imekuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi na kubadilisha maisha yao kama inavyoelekezwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha kuwa kila fedha inayopatikana inaelekezwa kwenye maendeleo ya watanzania” alisema Dkt. Nchemba.

Aidha, Dkt. Nchemba aliipongeza Kampuni hiyo kwa kuendelea kuboresha huduma zake na kuiwezesha kupanda kwa kushika soko la mawasiliano ya simu kutoka nafasi ya tatu hadi nafasi ya pili nyuma ya Kampuni ya Vodacom na kwamba hatua hiyo itaiwezesha Kampuni hiyo kuendelea kupiga hatua zaidi.

Alitoa wito kwa Kampuni hiyo na Kampuni nyingine za mitandao ya simu kutoa maoni ya namna ya kuboresha masuala ya Bajeti ya Serikali wakati huu ambapo Kikosi kazi cha masuala ya kodi kinaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine mbalimbali ili kuboresha ukusanyaji na matumizi ya Serikali kwa mwaka mpya wa Fedha wa 2022/2023.

Awali, akitoa taarifa fupi kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania aliyemaliza muda wake, Bw. George George Mathen, alisema katika kipindi chake cha miaka miwili na nusu cha kuongoza kampuni hiyo alifanikisha kutoa gawio na malipo mengine kwa Serikali yenye thamani ya shilingi bilioni 122.

“Kati ya fedha hizo, sh. bilioni 42 ni gawio kutokana na Serikali kumiliki hisa kwenye Kampuni, sh. bilioni 44 ni malipo baada ya kuhamisha umiliki wa minara yake kwenda Kampuni ya Minara pamoja na kiasi kingine cha sh. bilioni 34 zinazotokana na malipo ya kila mwezi ya sh. bilioni 1 kwa Kampuni hiyo ya Minara tangu ilipoingia nayo makubaliano ya kuendesha minara ya mawasiliano kuanzia Mwezi Aprili mwaka 2019” alieleza Bw. Mathen.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Airtel Tanzania, Bi. Beatrice Singano, aliipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini hatua iliyofanikisha Kampuni yao kupata faida na kutoa gawio kwa wanahisa wake ikiwemo Serikali.

Alisema wameshuhudia hatua kubwa iliyopigwa na Serikali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu yakiwemo madarasa na kwamba Airtel Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kupitia uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wake Mhe. Samia Suluhu Hassan na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za mawasiliano kwa njia ya kidijiti kwa asilimia 85 hivi karibuni.