Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), kumleta mhandisi mara moja kwenye mradi wa jengo la abiria linaloendelea kujengwa katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza.
Amesema jengo hilo la abiria linalojengwa kwa gharama ya takribani shilingi Bilioni 11 halijakidhi viwango vya kimataifa na kuna makosa mengine yanayohitaji watalaam zaidi kuweza kushauri namna gani ifanyike ili ikidhi viwango hivyo.
Prof. Mbarawa amesema hayo jijini Mwanza wakati alipofika kukagua ujenzi wa jengo hilo unaoendelea ambao mpaka sasa umefikia asilimia 85 na kutoridhishwa na mradi huo ambapo amesisitiza kuwa mradi huo umekosa vigezo vya kimataifa vinavyosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Anga (ICAO).
“Mwenye dhamana ya viwanja vya ndege sio Mkoa wala Halmashauri bali ni TAA, nashangaa kusikia hakuna mhandisi anayesimamia jengo hili kutoka kwao hivyo basi naagiza watoke Dar es Salaam waje kusimamia hili jengo ili tupate thamani ya fedha na viwango vinavyostahili, hatutaki kufanya makosa alafu badae tuje tulaumiane”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa majengo yanayostahili kujengwa katika viwanja vya ndege vya kimataifa ni tofauti na majengo mengine kwani yana viwango vyake vinavyostahili ambapo hapa havikufatwa.
“Tunatakiwa kujenga jengo liatakalodumu miaka 20 hadi 30 hatuwezi kujenga hivi hivi tu hapa tulipofikia wataalam waje waangalie nini kiboreshwe ili jengo likidhi mahitaji”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha viwanja vingi vya ndege hapa nchini na hiki Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kinatarajiwa kuwa cha Kimataifa hivyo lazima fedha zinazotolewa thamani yake ionekane na kupitishwa kwa viwango vya Shirika la Kimataifa la Anga (ICAO).
“Sisi kama Serikali tutahakikisha fedha zinaletwa ila mwisho wa siku tunahitaji kuona thamani ya fedha na kila anayehusika asimame kwenye eneo lake”, amesema Prof. Mbarawa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameeleza kuwa Mkoa imekwishaunda timu ya watalaam na tayari wameshaleta specification, michoro sahihi na kazi zinanedelea za kuboresha jengo hilo ili likidhi viwango vinavyostahili.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Miundombinu wa mkoa huo, Mbunifu Majengo Chagu Nghoma, amemueleza Waziri kuwa jengo hilo la abiria litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria laki nne kwa mwaka,
Ameongeza kuwa jengo litakuwa na ukumbi wa abiria wa ndani, wa kimataifa, ukumbi wa abiria mashuhuri, migahawa na maduka, ofisi mbalimbali za TRA, Uhamiaji, Afya, Polisi, Maliasili, Watumishi mbalimbali pia litakuwa na eneo la kuegesha magari takribani 320.
Ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ulianza mnamo tarehe 19/09/2021 na unatarajiwa kukamilika mwakani 2022.