Wananchi Muhimbili ‘wafunguka’ Mbele Ya Waziri Gwajima
Na Atley Kuni, WAMJW, DSM.
Wananchi na wazazi wanaopata huduma kwenye kliniki ya watoto katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamemuomba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuongezewa wataalam wa huduma ya mishipa ya ubongo.
Wakizungumza mbele ya Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima mara baada kufanya ziara ya kutembelea kliniki ya watoto kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, na kuzungumza na wananchi na watoa huduma kisha kupokea maoni ya wazazi aliwaokuta wakipata huduma ndani ya kitengo hicho, wazazi hao wamemuomba yafanyike maboresho kwenye eneo la huduma za vyoo kwa ajili ya kuwasitiri watoto wadogo, kuwekewa feni ili upunguza joto kwa watoto wadogo, kuongezewa mabenchi ya kukalia.
“Mhe. tunaomba kuongezwa kwa wataalam wa huduma ya mishipa ya ubongo kwani uhitaji mkubwa” alisema mmoja ya wananchi hao.
Kitengo hicho cha Mishipa ya fahamu pamoja na Ubongo, takwimu zinaonesha kinahudumia hadi Watoto 80 kwa siku, Idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na Idadi ya Mabingwa waliopo kwa sasa.
Akijibu maswali ya wananchi na wazazi hao Dkt. Gwajima alisema ameyapokea maoni na mapendekezo yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi.
“Ndugu zangu nimewasikia, uzuri hapa tupo na Mkurugezi anawasikia pia, lakini kama haitoshi, naomba niwape namba yangu ya kunitumia ujumbe mfupi, hii sio kwa ajili ya kupiga, niandikie ujumbe, tushauri nini tuweze kuboresha, kwa kutumia wataalam wetu tutachukua maoni yenu na tutayafanyia kazi” amesema Dkt. Gwajima.
Katika hatua nyingine, Waziri amemuelekeza Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufanyie kazi maboresho ambayo wananchi waliomba kuboreshewa, sambamba nakuendelea kuchukua maoni zaidi kwenye maeneo mbalimbali ambayo yatawasilishwa na wananchi ili huduma ziweze kuboreshwa.
Akizungumza wakati wa ziara, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Prof Laurence Museru aliahidi kuyafanyia kazi maboresho hayo, ambayo wananchi waliwasilisha ili kuweza kutatuliwa sambamba na kuongeza wataalam Bingwa wa masuala ya matatizo ya watoto ya Ubongo Pamoja na mishipa ya fahamu.
“Mhe. Waziri tumeyachukua haya ambayo wananchi wamewasilisha mbele yako, lakini mkakati mwingine tulionao ni kuongeza wataalam wabobezi kwa kuwapeleka shule ili wakihitimu waweze kusaidiana na hawa waliopo na kuondoa kabisa mapungufu haya ama kuyapunguza kwa asilimia kubwa. Prof. Mseru
Awali kabla ya kuwatembelea na kuzungumza wananchi hao waliofika kwa ajili ya huduma za kitabibu, Waziri Dkt. Gwajima, alifanya kikao cha Pamoja na Uongozi wa Hospitali hiyo kwa lengo la kukumbusha wajibu na kuweka mikakati ya uboreshaji wa huduma zinazo tolewa na Hospitali hiyo ya Taifa nchini.