Serikali ya Burundi siku ya jana imesema wafungwa 38 wamekufa baada ya kuzuka kwa moto mkubwa alfajiri ya leo na kuiteketeza jela moja kwenye mji wa Gitega ambao ni makao makuu ya serikali ya nchi hiyo.
Makamu wa rais wa Burundi Prosper Bazombanza ndiye ametangaza vifo hivyo baada ya kulitembelea eneo mkasa huo na kusema wafungwa wengine 60 wamejeruhiwa na kuna wasiwasi idadi ya vifo huenda itaongezeka.
Wengi ya wafungwa walikuwa wamelala wakati moto ulipozuka na mfungwa mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hata baada ya moto kusambaa polisi walikataa kufungua milango ya vyumba vya gereza.
Wizara ya mambo ya ndani imesema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotokea ndani ya gereza hilo kongwe ambalo hadi mwezi Novemba lilikuwa na kiasi wafungwa 1,500.