Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuwa utoaji wa chanjo za nyongeza ni suala la dharura na muhimu ili kupambana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona kote barani humo na kuzuka kwa aina mpya ya kirusi cha Omicron. 

Huku msimu wa siku kuu ukikaribia, viongozi wa ulaya pia wamesisitiza umuhimu wa hatua iliyoratibiwa ili kuepusha hali ya kutatanisha ya sheria katika nchi 27 wanachama, na kuhakikisha kuwa vyeti vya COVID-19 vinaendelea kuwaruhusu watu kusafiri bila vikwazo. 

Viongozi hao waliokutana mjini Brussels, wamesisitiza kuhusu haja ya kuwepo na mbinu iliyowianishwa ili kuepusha vikwazo kwa usafiri huru kati ya nchi wanachama au kuathiri safari katika kanda hiyo. 

Ufaransa kuanzia Jumamosi itaweka vikwazo vikali kwa wasafiri wanaotokea Uingereza kutokana na kirusi cha Omicron. Italia, Ureno na Ugiriki pia zimeweka kanuni kali kwa wanaowasili nchini humo.