Ufafanuzi Kuhusu Madai Yaliyotolewa Na Chama Cha ACT-Wazalendo Kuhusu Ukiukwaji Wa Haki Za Binadamu Katika Msitu Wa Makere
Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa kwa umma iliyotolewa na Chama cha ACT – Wazalendo ikiwa imeambatishwa picha inayoonesha mtu anayedaiwa kujeruhiwa kwa kukatwa vidole vya mkono na askari wa Uhifadhi wanaolinda msitu wa Makere wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Ukweli ni kwamba mwanzoni mwa mwezi Oktoba, 2021 zilitolewa taarifa katika kituo kidogo cha Polisi Makere wilayani Kasulu za vijana wawili waliodai kujeruhiwa kwa kukatwa vidole na askari wa Uhifadhi.
Kufuatia taarifa hiyo timu ya upelelezi kutoka Kikosi cha Kupambana na Ujangili cha Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na maafisa wa TFS walifuatilia tukio hilo mara moja. Aidha, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kasulu iliunda kamati iliyohusisha pia viongozi wa Kijiji cha Mvugwe ambacho vijana hao walikuwa wanatoka ili kufuatilia tuhuma hizo sambamba na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo.
Ili kubaini ukweli wa chanzo na wahusika wa tukio hilo hatua mbalimbali za upelelezi zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhoji wananchi, maafisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA). Aidha, gwaride la utambuzi lilifanyika tarehe 23 Oktoba 2021 kwa mujibu wa sheria ambao jumla ya askari 10 (3 waajiriwa wa TFS na 7 waajiriwa wa SUMA JKT wanaofanya kazi na TFS) walishiriki ili vijana hao waweze kuwatambua watuhumiwa wa tukio hilo zoezi ambalo lilikamilika bila vijana hao kuwatambua askari wanaodai kuwa walihusika katika kitendo hicho.
Aidha, uchunguzi uliofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama ulibaini kuwa walalamikaji hao wawili ambao ni Bw. NZEYIMANA Juma (miaka 27) na Bw. TUYISENGE, Elia (Miaka 30) walikuwa ni wakulima na wakazi wa maeneo ya Rumonge na Luligi kutoka nchi jirani ya Burundi. Mbali na uchunguzi huo hakukua na ushahidi wowote ulioonesha kuwa vijana hao walijeruhiwa wakiwa ndani ya eneo la hifadhi ya msitu huo.
Jeshi la Uhifadhi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani Kigoma linaendelea kufuatilia tukio hilo na matukio mengine ya aina hiyo ili kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaobainika kukiuka sheria za nchi.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa wananchi wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wanaendelea kuzalisha mazao ya chakula na kunufaika na shughuli za kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TFS ilitekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa tarehe 21 Julai, 2017 akiwa ziarani mkoani Kigoma la kuwapatia wananchi wa wilaya ya Kasulu sehemu ya msitu wa hifadhi Makere Kusini ili watumie kuzalisha mazao ya chakula.
Katika mpango huo jumla ya hekta 10,012.61 zilimegwa kutoka kwenye msitu huo ambapo hekta 2,496 (sawa na ekari 6,167.7) zitolewa kwa ajili ya matumizi kwa wananchi wa kata ya Kagerankanda, Kijiji cha Mvinza hekta 2,174 (sawa na ekari 5,371.9) na hekta 5,342.61 (sawa na ekari 13,201.88) ambazo ziko chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya watu wengine toka kwenye vijiji vingine watakaokuwa na uhitaji wa ardhi ambalo limepangiwa matumizi bora ya ardhi.
Ili kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo hayo wanashiriki ipasavyo walioneshwa ardhi yao na mipaka ikawekwa katika maeneo yote. Hata hivyo, kumekuwa na changamoto ya wananchi kuingia kufanya shughuli za kibinadamu hususani kilimo na kuchunga mifugo ndani ya msitu nje ya maeneo waliyotengewa kisheria. Tathmini inaonesha mahitaji ya ardhi ya kilimo hayatokani na wananchi wanaozunguka msitu huo bali wageni wanatoka nje ya wilaya na mkoa wa Kigoma ambao huingiza makundi makubwa ya wafanyakazi kufanya shughuli hizo ikiwa ni pamoja kufanya uwindaji haramu wa wanyamapori. Hivyo, serikali inatoa wito kwa wananchi kuheshimu mipaka iliyowekwa na kufanya shughuli zao katika maeneo waliyopewa kisheria.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuheshimu Sheria na Utu katika kushughulikia masuala yote yanayohusu usimamizi wa rasilimali za misitu na maliasili nyingine hapa nchini.