Tanzania Yasisitiza Kuunga Mkono ,kuendeleza Uhusiano Na China
Tanzania imesisitiza kuunga mkono, kuendeleza ushirikiano, uhusiano na mshikamano ambao China umekuwa ukiuonesha kwa nchi za Afrika.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula alipozungumza katika Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30, 2021.
Amesema kwa kuangalia yaliyotokea katika kipindi hiki kigumu ambacho dunia inakipitia , China imekuwa ikishirikiana na Afrika kwa kutoa misaada mikubwa kwa nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali na kuwa na ushirikiano ambao umetunufaisha pande zote.
Amesema kwa upande wa Tanzania China imekuwa ikisaidia katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imekuwa ikifanyika kwa kushirikiana na makampuni yao makubwa yanayowekeza chini .
Aidha Tanzania imeiomba China kuweka msisitizo mkubwa katika sekta ya afya hasa katika kupambana na janga la ugonjwa wa korona unaosababishwa na virusi vya COVID 19 kwa kujengewa viwanda na kupatiwa uwezo wa kuzalisha chanjo hizo na dawa nyingine wenyewe.
Waziri Mulamula amepongeza kauli ya Rais wa China Mhe. Xi Jinping ya kuwa nchi hiyo itatoa dozi billioni moja zaidi kwa nchi za Afrika ili kuziwezesha nchi za Afrika kufikia lengo la kutoa chanjo kwa angalau asilimia 60 kwa watu wake ifikapo mwaka 2022.
“Tanzania imepokea taarifa hizo kwa mikono miwili na tunaishukuru serikali ya China kwani iliipatia Tanzania chanjo laki tano na tunategemea kupata chanjo nyingine, na sasa kwa tangazo hilo China wametuhakikishia kwamba tutapata chanjo kwa kiasi kile tunachohitaji”, amesema Balozi Mulamula.
Mkutano huo ulijumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China na kuangalia ambavyo China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu cha 2018-2021 kwenye maeneo ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda barani Afrika, ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano, kukuza wigo wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.
Maeneo mengine ni kampeni ya mapinduzi ya kijani, mpango maalum wa mafunzo ya ufundi, kuboreha sekta ya Afya, ulinzi na usalama na ushirikiano katika masuala ya habari, utamaduni sanaa na michezo.