Serikali Yatoa Zaidi Ya Sh.524 Milioni Kujenga Barabara Wilayani Iramba
Na Dotto Mwaibale, Iramba Singida
SERIKALI imetoa Sh.524,448,800 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Shelui-Tintigulu yenye urefu wa kilomita 7.3 katika Kata ya Shelui wilayani Iramba mkoani Singiga.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Iramba, Evance Kibona wakati akitoa taarifa mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu katika ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua miradi ya maendeleo aliyoifanya leo.
Kibona alisema mradi huo unatekelezwa kwa fedha za tozo kutoka Serikali Kuu na ujenzi wa barabara hiyo unafanywa na Kampuni ya M/s Jp Traders Limited ya jijini Dar es Salaam na kuwa ujenzi huo ulianza rasmi Desemba 11, 2021 na unakadiriwa kukamilika Juni 10 mwakani.
"Mradi huu umelenga kufungua barabara ambapo ujenzi wa kivuko kwenye mto Kinshoka utazingatiwa awamu nyingine kadri bajeti itakavyoruhusu" alisema Kibona.
Kibona alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia sana kufungua mawasiliano na hivyo kurahisisha usafiri katika shughuli za kiuchumi na kijamii kati ya vijiji 6 vya Nselembwe, Tintigulu, Wembere, Kibigiri, Ntwike na Shelui vya Kata ya Shelui na Ntwike vyenye jumla ya wakazi 14,933.
Alisema vijiji vyenye wakazi hao vinajishughulisha na shughuli za kilimo na ufugaji.
Kibona alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya miundombinu ya barabara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo mradi huo ni sehemu ya ongezeko hilo.
Waziri Ummy Mwalimu baada ya kupokea taarifa hiyo aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kuomba fedha mwaka wa fedha 2021/2023 Serikali Kuu kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa daraja la Kinshoka ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.
Mkazi wa Kijiji hicho Neema Mathayo aliishukuru Serikali kwa kuwajengea barabara hiyo ambayo itakuwa ni mkombozi kwa kuwa walikuwa na changamoto kubwa ya kupata usafiri wa kwenda kwenye shughuli zao za kiuchumi hasa wanawake wakati wa kwenda Hositali kwa ajili ya kujifungua.
Katika ziara hiyo Waziri Ummy alikagua barabara hiyo, ujenzi wa madarasa kupitia fedha za Uviko 19, mradi wa ujasiriamali wa Wasichana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iramba na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Kisiriri ambapo pia alizungunguza na Watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.