Rais Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) utakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, ili uweze kuleta tija kwa Watanzania.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli hiyo awamu ya tatu kipande cha kutoka Makutupora hadi Tabora, Rais Samia amesema Serikali imewekeza takribani shilingi trilioni 14 .7 kwenye mradi huo, hivyo ni lazima uwe ni wenye maslahi kwa Taifa.
Rais Samia Suluhu Hassan ametumia hafla hiyo kusisitiza kuwa miradi yote mikubwa inayotekelezwa na Serikali itakamilika kwa wakati uliopangwa, ili Wananchi waweze kunufaika.
“Niliahidi kuendeleza mema yaliyopita, yaliyopo na kuanzisha mema mapya. Ujenzi na utekelezaji wa miradi yote iliyoanzishwa na inayoendelea…, tutaendelea kuisimamia na kuhakikisha inakamilika. Sasa kuna wale ambao walipenda kuona miradi hii haiendelezwi na wanathubutu kusema kwamba miradi hii imeshindikana, haiendelezwi.
“Pamesemwa hapa makandarasi hawadai hata senti moja ila Serikali inadai kazi, hivyo hivyo kwa miradi mikubwa mingine. ujenzi wa bwawa tunakwenda nao vizuri hatudaiwi na miradi mingine yote iliyoachwa tunakwenda nayo vizuri.
“Na mkipita pita huko hakuna mradi uliosimama, miradi yote inaendelea. Nataka kuwaambia Watanzania tutasimamia miradi iendelee…, kwa hiyo kama walidhani kutakuwa na kusimamishwa miradi ili wapate la kusema halipo. Tutaendelea na ujenzi wa miradi, kuna jitihada za kutuvunja moyo katika mikopo, hata hizo nchi zilizoendelea zina mikopo mikubwa kuzidi ya kwetu…,tutakopa tumalize miradi ya maendeleo,” amesisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa SGR awamu ya tatu kipande cha kutoka Makutupora hadi Tabora utagharimu zaidi ya shilingi trilioni 4.4 na ujenzi wake utakuwa wa muda wa miezi 46.
Mradi wa Reli ya kisasa awamu ya tatu kipande cha kutoka Makutupora hadi Tabora kina urefu wa kilomita 368.