Na WAMJW-DSM
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea Dozi 376,320 za Moderna ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha ikiwakinga Wananchi wake dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Hafla fupi ya mapokezi imefanyika 24 Disemba 2021 na kuongozwa na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Ubalozi na Taasisi zisizo za kiserikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Gwajima amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imelenga kuwakinga jumla ya Watanzania 249,795 kutokana na kupokea Chanjo dozi 376,320 za Moderna zilizoingia kupitia mpango wa COVAX Facility zitakinga watanzania 188,160 ikiwa ni awamu ya kwanza kupokea aina ya Chanjo za Moderna.

"Mapokezi ya chanjo hizi za leo yanafanya jumla ya chanjo tulizopokea hapa nchini tangu tuanze kutoa chanjo za chanjo dhidi ya UVIKO 19 hadi sasa zimefikia dozi 6,408,950 zikijumuisha (Sinopharm, Janssen, Pfizer), na leo Moderna ambazo zinatosha kuchanja jumla ya watanzania 3,204,475
hivyo niwaombe wanaohusika na zoezi hilo kuwajibika kwa kasi kubwa ili kuwawezesha watanzania wengi kupata chanjo mapema iwezekanavyo amesema Mhe.Dkt Gwajima.

Aidha,Mhe.Dkt.Gwajima amesema kuwa Wizara imetoa Mwongozo wa Chanjo unaofafanua vyema taratibu za utoaji wa chanjo hizi wenye lengo la kufikia uchanjaji wa asilimia 60 ya watanzania ili kudhibiti ugonjwa wa uviko 19.