Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WFM, Mwanza
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewaagiza watendaji na watalaamu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kuongeza bidii katika kufanya tafiti zitakazo changia kuondoa umasikini na kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yameelezwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA  Leonard Mkude, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), katika mahafali ya 35 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini na ya tisa kwa upande wa Kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoani Mwanza.

CPA Mkude alisema kuwa ni jambo la kufurahisha na kutia moyo kuona Chuo kinatekeleza kwa vitendo moja ya majukumu yake ya msingi ya kutoa huduma ya ushauri elekezi kwa jamii, Halmashauri na Taasisi mbalimbali.

‘’ Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kuunga mkono juhudi za ujenzi wa Chuo cha Mipango kwa kuendelea kutoa fedha za Maendeleo na kuweka msukumo ili kiendelee kujenga majengo ya kisasa yanayokidhi mahitaji’’alisema CPA Mkude.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha Miaka hii 60 nchi imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja ya elimu, ikiwemo ongezeko kubwa la shule za msingi, sekondari , vyuo vya kati, na vyuo vya elimu ya juu na kuwa Serikali itaendelea kujenga vyuo vya ufundi katika kila Mkoa ili kutoa fursa kwa Vijana wanaomaliza elimu ya Sekondari na Msingi kupata ujuzi.

CPA Mkude aliupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuwekeza katika ushirikiano na wadau wa maendeleo wakiwemo UNDP, FAO, UNICEF, NUFFIC, EU, AGRA na wengine, katika mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umasikini pamoja na kuwezesha kutoa huduma ya ushauri elekezi kwa jamii.

Aidha, aliwaasa wahitimu kutumia  ujuzi, elimu, na maarifa waliyoyapata chuoni hapo kwa manufaa ya umma kwa kuanzisha vikundi  vya uzalishaji mali kwa kutumia  fursa ya mikopo nafuu inayopatikana katika halmashauri nchini.

Pia alitoa wito kwa waajiri  na wadau wote wa maendeleo nchini kuwatumia vijana hao ambao wameiva na kubobea katika fani ya  mipango ya maendeleo ambayo ni muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote duniani.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Prof. Hozen Mayaya, aliishukuru Serikali kwa jinsi inavyotenga fedha za Maendeleo ambazo zimesaidia kujenga majengo ya chuo hicho katika eneo la Kitumba “A” Kata ya Kisesa, wilayani Magu, ambapo mahafali ya mwaka huu yamefanyika hapo kwa mara ya kwanza.

Alisema kituo cha mafunzo Kanda ya Ziwa Mwanza kimekuwa na ongezeko la udahili kila mwaka sambamba na ongezeko la Wahitimu ambapo Mahafali ya Kwanza ya Mwaka 2011/12 kulikuwa na jumla ya Wahitimu 269, ilihali mwaka huu kuna jumla ya Wahitimu 2718.

‘‘Ili kuongeza wigo wa fursa za ajira miongoni mwa wahitimu wetu, Chuo kimeanzisha kituo cha ubunifu na ujasiliamali, ambapo wanafunzi wanapata nafasi ya kujifunza masuala ya ubunifu na ujasiriamali, hivyo kuwa tayari kuajiriwa na kujiajiri’’,Alisema Profesa Mayaya.

Alisema kuwa chuo kupitia timu ya wataalamu wake kimefanikiwa kundika maandiko yaliyo pata ufadhili kutoka katika mashirika ya Kimataifa, yakiwemo UNICEF, EU, AGRA na UNDP, na kutekeleza mradi uliofadhiliwa na UNDP, wa namna ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi na Kupunguza Umasikini katika jamii za Kanda ya Ziwa.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Martha Qorro, alisema kuwa wataendelea kukisimamia chuo kwa weledi ili kiweze kufikia malengo ya kuanzishwa kwake kwa kusimamia utekelezji wa Mpango Mkakati wa Chuo 2021/22 hadi 2025/26 ambao umepitishwa mwaka huu.

‘Tunakuahidi kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu ili Chuo kiendelee kutekeleza majukumu yake ya msingi na ya maendeleo kwa kufuata kanuni, miongozo, sheria na taratibu zilizopo na zitakazotolewa mara kwa mara na mamlaka’ alisema Profesa Qorro.

Mahafali ya mwaka huu ya chuo hicho kwa Kanda ya Ziwa ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza katika majengo mapya ya chuo hicho yamehusisha Wahitimu 2718 wakiwemo wanaume 1,086 na wanawake 1,632 katika fani mbalimbali.