“Serikali Ya Rais Samia Imejipanga Kuimarisha Sekta Ya Viwanda Na Biashara “ -Dkt.Hashil Abdalah
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdalah amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuimarisha sekta ya viwanda na biashara kwa kuhakikisha wafanyabiashara wananufaika na Serikali inanufaika kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo alipokuwa akifungua maonyesho ya bidhaa za usafirishaji ambazo zinaingizwa nchini kutoka India katika hafla fupi iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wanahabari, wafanyabiashara na wananchi waliofika katika maonyesho hayo Dr. Abdallah amesema Maonyesho hayo ni muhimu katika kukiza uchumi wa nchi kwa kuwa vifaa vya usafirishaji kama Pikipiki, Bajaji, Matrekta magari vinatumiwa na wananchi wengi katika kurahisisha shughuri zao za kila siku.
“Bidhaa hizi mfano Matrekta, Bajaji, Pikipiki zinaingia sokoni kama mitaji ambayo inatumika na watu kujiendeleza kiuchumi ” Amesema Dkt. Absallah.
Aidha, Dkt. Abdallah amesema Wizara ya Viwanda na Biashara ipo tayari kutoa ushirikiano na kutatua changamoto ambazo zinawakabili wafanya biasharawakati wowote kwa kushirikiana na wadau wengine.
Naye, Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema ingawa kwa sasa bidhaa hizi zinazalishwa nchini India, hivi karibuni zitaanza kuzalishwa nchini Tanzania.
Dkt. Abdallah ametoa rai kwa watanzania kufika katika maonyesho hayo kuzungumza moja kwa moja na wafanyabiashara na benki zilizopo hapo ili kuona namna ya kutumia fursa hii kujinufaisha.