WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa kamati za amani za viongozi wa dini zinazojumuisha dini zote na ambazo tangu kuanzishwa kwake, zimechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha amani nchini.

Amesema amani ambayo imekuwepo nchini tangu kupata uhuru imechangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa dini pamoja na Kamati za Amani za viongozi wa dini. “Upendo, utaifa na mshikamano ni mambo ya msingi kabisa katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumapili, Desemba 5, 2021) wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya Buddhism barani Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa viongozi, wafuasi na marafiki wa Buddha kwamba wanapoadhimisha miaka 100 ya Ubuddha barani Afrika, waendelee kuvumiliana na kustahimiliana hususan pale zinapotokea sintofahamu miongoni mwao.”

“Ninakupongeza sana wewe binafsi, Kiongozi wa Buddha Afrika ukiwa mjumbe wa kamati ya amani ya kitaifa na viongozi wengine wa dini kwa mchango mkubwa mnaoutoa kupitia kamati ya amani za kitaifa. Ninatambua kuwa katika kipindi cha takriban miaka 22 tangu kuanzishwa kwa kamati za amani, umekuwa miongoni mwa wadau wake muhimu.”

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amesifu taasisi za kidini za wabuddha ambazo zinatoa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo kuwahudumia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wasiopungua 100 katika kituo cha watoto yatima cha Chanika Children’s Shelter.

“Ninatambua kuwa kupitia taasisi yenu ya Kind Heart Africa Charitable Organization mmeendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma za kijamii nchini. Juhudi hizo zinajidhihirisha kupitia mradi wa Chanika Children’s Shelter (CCS) mnaoutekeleza kwa ubia na Human Welfare Trust (HWT).”

“Nimefahamishwa pia kuwa mpo mbioni kuanzisha huduma za afya pamoja na kutoa huduma za malazi na chakula kwa wazee. Hongereni sana kwa moyo huo wa upendo kwa jamii yetu.”

Akizungumzia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 wenye thamani ya sh. trilioni 1.3, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mpango huo utaimarisha miundombinu ya afya, elimu, maji, utalii, maeneo ya biashara za wajasiriamali wadogo, uwezeshaji wa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na kaya maskini.

Amesema kuwa katika kipindi cha miezi 9 ya utekelezaji wa mpango huo, jamii inayoishi kwenye mazingira magumu zikiwemo kaya maskini imetengewa sh. bilioni 5.5. “Pia shilingi bilioni tano zimetengwa ikiwa ni sehemu ya kuwezesha makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili waweze kujikwamua kiuchumi.”

Awali, Mtawa Mkuu wa Buddha Bara la Afrika, Mchungaji Dkt. Iikupitiye Pannasekara, aliipongeza Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa kuendelea kudumisha amani na upendo miongoni mwao licha ya kuwa na dini tofauti.

“Tanzania ni nchi ya kuigwa pamoja na ukarimu wao bado, Serikali na wananchi wake wameendelea kudumisha amani. Hakuna mifarakano wala ugomvi wa kidini miongoni mwetu, wote tunaishi kama ndugu, katika kipindi hiki ambacho tunatimiza miaka 100 tunajisikia faraja kuwa sehemu ya amani hii miongoni mwa Watanzania.”