Serikali imesema haitavumilia vitendo vya rushwa ya ngono katika Taasisi za elimu kwani ni ukosefu wa maadili na vinashusha heshima ya wanataaluma pamoja na taaluma katika taasisi hizo.
 
Kauli hiyo imetolewa Desemba 07, 2021 Jijini Dare es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati alipokuwa akizindua siku ya afya ya akili iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo amesema  vitendo hivyo vinapaswa kukemewa kwa nguvu zote na kuchukuliwa hatua mara moja pale inapobainika mtumishi yeyote ameshiriki vitendo hivyo.
 
Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi wa kike katika taasisi za elimu wanapokutana na kadhia ya rushwa ya ngono kutokukubali kuingia katika mtengo huo na badala yake watoe taarifa kwa idara na vitengo vinavyohusika na ushauri na unasihi katika taasisi hizo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wahusika.
 
“Sisi kama serikali tunasikitika sana tunapoona na kusoma katika vyombo vya habari taarifa za watoto wetu wa kike katika taasisi za elimu wananyanyasika kwa vitendo hivi vya rushwa ya ngono, nawaomba sana binti zetu msisite wala kuogopa kutoa taarifa ili tuweze kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahusika na kuwalinda msikubali kunyanyasika kwa ajili ya maumbo yenu” amesisitiza waziri huyo.
 
Aidha, Waziri Ndalichako amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuanzisha Kitengo cha Ushauri na Unasihi chini ya Kurugenzi ya Huduma za Jamii kwa nia ya kuwasaidia wafanyakazi na wanafunzi kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo msongo wa mawazo, sonona, utendaji kazi chini ya kiwango, utoro na ukiukwaji wa miiko na maadili ya kazi.
 
Prof. Ndalichako ametaka kitengo hicho kufanya kazi kwa uaminifu ili kiaminika na kuwapa wanafunzi nafasi salama ya kueleza changamoto zote ikiwa ni pamoja na rushwa ya ngono ambapo amesema kama kazi ya ushauri na unasihi ikifanyika kwa ukamilifu hakutakuwa na matatizo ya rushwa ya ngono vyuoni na kwenye taasisi za elimu.

Hivyo ameagiza wanasihi na washauri wote wanaofanya kazi katika kitengo hicho kuwa wataalam ambao wamebobea, wenye usiri na wanaofanya kazi yao kitaalamu na kuwa na utendaji kazi utakaomfanya muathirika awaone kama kimbilio badala ya kuwakimbia.

Pia Prof. Ndalichako amesema kuwa hata katika ngazi za shule ya msingi na sekondari tayari serikali imeshaimarisha vitengo vya ushauri na unasihi pamoja na kutoa mwongozo wa namna vinavyopaswa kufanya kazi kwa kuwa hata katika ngazi hizo kuna wanafunzi wanapata changamoto mbalimbali zinazopelekea kukatisha masomo yao.
 
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Profesa Bonaventure Rutinwa amesema kuanzishwa kwa kitengo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Ushauri na Unashii ya chuo hicho na kufanya kuwa Chuo cha kwanza kuwa na kitengo cha namna hiyo ambapo amesema mpaka sasa kimeshatoa ushauri na unasihi kwa wanafunzi na watumishi mbalimbali ambapo imewawezesha kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo.