Rais wa zamani wa Afghanistan Ashraf Ghani amesema hakuwa na chaguo jingine ila kuondoka haraka Kabul wakati Wataliban waliukaribia mji huo mkuu. 

Ghani amekanusha kuwa kulikuwa na mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea wakati huo ya makubaliano ya kuwachia madaraka kwa amani, kama walivyodai maafisa wa zamani wa Afghanistan na Marekani. 

Katika mahojiano na shirika la utangazaji la Uingereza BBC, Ghani amesema mshauri wake alimpa dakika chache tu kuamua kuondoka Kabul. 

Pia amekanusha tuhuma zilizoenea kote kuwa aliondoka Afghanistan na mamilioni ya fedha za kuibwa. 

Rais huyo wa zamani hakuzungumzia kuanguka kwa kasi kwa jeshi la Afghanistan katika wiki za mwisho kabla ya kuwasili kwa Taliban mjini Kabul lakini aliyalaumu makubaliano ambayo Marekani ilisaini na Taliban mwaka wa 2020 akisema yalisababisha kuanguka kwa serikali yake.