Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wanatarajiwa kufanya mazungumzo kwa njia ya video siku ya Jumanne wakati mgogoro juu ya Ukraine ukiendelea kuongezeka. 

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alithibitisha mipango ya mazungumzo hayo kupitia shirika la habari la serikali ya Urusi RIA Novosti na Ikulu ya Marekani imesema viongozi hao watajadili masuala mbalimbali. 

Biden siku ya Ijumaa alisema atafanya iwe "vigumu sana" kwa Urusi kuanzisha uvamizi wowote dhidi ya Ukraine. Marekani na Ukraine zinasema kuwa Urusi imekusanya wanajeshi wengi karibu na mpaka wa Ukraine na kuishutumu Urusi kwa kupanga uvamizi. 

Urusi imekanusha nia yoyote mbaya na kushutumu nchi za Magharibi kwa uchochezi, haswa kwa shughuli za kijeshi katika Bahari Nyeusi, ambayo inaona kama sehemu ya nyanja yake ya ushawishi. Biden na Putin walitarajiwa kushiki mazumgumzo hayo tangu Ijumaa.