Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 5,704 kuachiwa huru katika kumbukizi ya miaka 60 ya sikukuu ya uhuru iliyofanyika Desemba 9, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Waziri wa Mambo ya ndani George Simbachawene amesema msamaha huo aliutoa Mhe. Rais Samia mwaka huu katika sherehe za maadhimisho hayo Kwa kutumia kifungu cha katiba ibara ya 9 ibara 45 (1)(d).

“Wafungwa wote wapunguziwe robo ya adhabu zao baada punguzo la kawada la moja ya tatu linatolewa chini ya kifungu cha 49(1) cha sheria yavmagereza sura ya 58 wafungwa hao sharti wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na wawe wameingia gerezani kabla ya Oktoba 9, mwaka huu isipokua wafungwa waliorodheshwa katika shari2(i_x)” amesema Waziri Simbachawene.

Waziri amesema msamaha huo umezingatia masharti ikiwemo kuwaachia wafungwa wagonjwa wenye ugonjwa wa kudumu na hawawezi kufanya kazi, wafungwa wazee, wenye umri wa miaka 70 au zaidi ya umri huo na uwe umethibitishwa na jopo la madaktari chini ya mganga mkuu wa mkoa au wilaya.

Aidha ameongeza kuwa wafungwa wengine watakaohusika katika msamaha huo ni wanawake walioingia gerezani na mimba, na wale walioingia gerezani na watoto wanaonyonya na wasionyonya watoto, wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili waliokaa gerezani zaidi ya miaka 20, wafungwa wenye miaka 15,walionyesha tabia njema.

Hata hivyo amesema msamaha huo hauhusishi wafungwa walio na makosa ya kunyongwa, wahujumu uchumi, utakatishaji wa fedha, usafirishaji dawa za kulevya, ukatili dhidi ya watoto, utoroshaji nyara za kiserikali, ubakaji, waliojaza wanafunzi mimba, wakitumia madaraka vibaya, rushwa.

Waziri Simbachawene amesema hii ni mara ya kwanza Rais kuwaachia wafungwa wenye umri mkubwa kuanzia miaka sabini na kuendelea hivyo amewaasa wafungwa wote waliopata msamaha huo wajutie makosa yao na wasirudie kufanya makosa tena

Aidha, Simbachawene amesema serikali itaweka utaratibu wa kuwafuatilia wafungwa walioachiwa kwa msahama wa Rais ili kuzuia wasiendelee kutenda makosa kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara.