Rais Samia Suluhu Hassan amesema, madini yanayochimbwa hapa nchini yataongezwa thamani hapa hapa nchini ili kuongeza pato litokanalo na sekta ya madini.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini wa mikataba baina ya Serikali na kampuni nne za uchimbaji madini Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, Serikali haitatoa kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi bali itaendelea kuyaongeza thamani hapa nchini kabla ya kuuzwa nje.

Ameongeza kuwa Serikali inaiangalia sekta ya madini kama sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi, na kwamba itaendelea kushirikiana na Wawekezaji katika sekta hiyo ili iweze kufikia lengo la kuchangia pato la Taifa kwa asilimia 10.

Kuhusu utoroshwaji wa madini, Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza wizara ya Madini pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya doria katika maeneo ya uzalishaji wa madini ili kuhakikisha kuwa hakuna utoroshwaji katika maeneo hayo.

Rais Samia Suluhu Hassan pia amezungumzia utunzwaji wa mazingira katika maeneo yanapochimbwa madini ambapo amezitaka taasisi zinazosimamia sekta hiyo kushirikiana na Wawekezaji ili athari za mazingira zisiwaumize wananchi.

Amewataka Wawekezaji kusimamia makubaliano ya kurudisha faida kwa Wananchi, badala ya kuwadhulumu na kuwafanya washindwe kupiga hatua katika maeneo ambayo wamewekeza.

Awali akimkaribisha Rais, Waziri wa Madini Dotto Biteko amesema kuwa uwekezaji unaofanywa na kampuni hizo 4 una thamani ya shilingi trilioni 1.5, jambo ambalo litachangia kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya madini.

Waziri Biteko ameongeza kuwa sekta ya madini imeongeza makusanyo yake kutoka shilingi Trilioni moja mwanzoni mwa mwaka huu hadi kufikia Trilioni 4 mwezi uliopita.