Rais Samia avunja bodi ya bandari, Shirika la Meli
Rais Samia Suluhu Hassan amevunja bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL) na kuagiza wizara kuichukulia hatua bodi ya manunuzi kwa kutoa tenda ya ujenzi wa meli 5 kwa kampuni ‘hewa’.
Maamuzi ya Rais Samia leo Dis. 4 yanafuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na timu maalumu aliyoiunda kuchunguza uhalali wa kampuni ya Uturuki, YÃœTEK iliyoshinda tenda kujenga meli tano za abiria na mizigo za kampuni ya Meli nchini.
Dau hili lenye thamani ya Sh bilioni 438.8 lilisainiwa mjini Mwanza Jun. 15, 2021 nakushuhudiwa na Rais Samia. Hata hivyo timu iliyohusisha wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Askari kutoka kikosi ya wanamaji, na wataalamu kutoka MSCL ilibaini kuwa YÃœTEK haikuwa na uwezo wa kifedha wala wataalamu kutekeleza mkataba huo.
“Nimeagiza Waziri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuvunja mkataba huo… hata hivyo uwezo wangu ni kuvunja bodi hivyo wenyeviti wote wawili nimewaondoa,” alisema Rais Samia wakati akizindua maboresho ya gati za Bandari ya Dar es Salaam.
Rais Samia amesema mkandarasi huyo alikuwa ameweka wakala nchini aliyekuwa anufaike kati ya Dola za Marekani milioni 1.9 hadi 2 kwa kila meli itakayo jengwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi, Mkandasi huyo hana eneo la kujenga meli (shipyard) badala yake wao ni madalali wa kutafuta kazi na kutoa kwa kampuni zingine. Pia ilibainika kwamba uwezo wa kampuni kifedha ni mdogo mno.
Wasifu na uwezo wake katika ujenzi ni wa mashaka kwani haipo hata kwenye orodha ya wajenzi wa meli inayotolewa na umoja wa wajenzi wa meli Uturuki. “Hili ndio liliotuthibitishia kwamba hawa ni madalali. hawakuwa na watu wenye sifa na vifaa vya kujenga meli. hadi sasa kampuni hiyo haijafanya lolote,” amesema Rais Samia.
Mkuu huyo wa nchi amehoji ikiwa uwezo wa kampuni hiyo ulikuwa ni kutengeneza boti ndogo.
“Tujiulize tenda hii ilitolewa na bodi husika ya wizara ama shirika. Shirika linabodi ya wakurugenzi ambao wamepitisha tenda hii lakini pia mkandarasi alifanyiwa due diligence. Sasa haya tumeyabaini hivi karibuni, huko nyuma yametokea mangapi?” alihoji nakutaka tenda bodi iliyohusika, bodi ya wakurugenzi kuwajibishwa.