Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia na kutii sheria ili kuepuka heshima zao kuondoka.

Rais Samia ameeleza hilo leo wakati akijibu ombi la Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe ambaye alimuomba awasaidie kumsamehe Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe.

''Nataka nizungumzie kidogo aliloniomba mwanangu Zitto, kwamba yule mwenzetu msamehe basi aje awe na sisi. Demokrasia ni kuheshimu sheria, heshima ya mtu inakuja kwa kuheshimu sheria za nchi.,'' ameeleza Rais Samia Suluhu.

Ameendelea,’’Isingekuwa uvunjifu wa sheria leo isingemlazimu Zitto kuomba hapa kwamba yule mwenzetu muachie lakini unapovunja sheria unajivunjia heshima

“Naomba tufanye kazi kwa kuheshimu sheria, waswahili wanasema mtaka nyingi nasaba hupata mingi misiba, ingawa kusameheana nako kupo,” amesema Samia.

Aidha Rais Samia amesisitiza kuwa kuna taifa moja tu ambalo raia wote wanawajibika kulilinda.

''Nitumie fursa hii kuwakumbusha kwamba Duniani kuna nchi moja tu inayoitwa Jamhauri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni taifa huru lililojengwa kwa misingi ya amani, upendo,  mshikamano na linaloongozwa kwa misingi ya katiba na sheria zilizotungwa na bunge na sio utashi wa mtu au mataifa mengine. Na wenye hili taifa ni sisi,'' amesema Rais Samia Suluhu.