Kumekuwa na changamoto ya kuwepo kwa mianya mingi ya upotevu wa mapato inayotokana na kukataa kwa makusudi kuweka mifumo madhubiti ya ukusanyaji mapato na mifumo inayosomana baina ya Bandari na Mamlaka ya Ukusanyaji Mapato Tanzania (TRA).

Mapato katika Bandari ya Dar es Salaam yamekuwa yakipanda na kushuka na kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20, Bandari ilikusanya Sh bilioni 901, mwaka 2020/21 ilikusanya Sh bilioni 896 na matarajio ya 2021/22 ni kukusanya Sh bilioni 980.

“Hizi Mamlaka mbili hazisomani mifumo yao. Kuna utata mwingi. kuna mifumo kadhaa na kila mfumo na mambo yake kiasi ambacho kinaruhusu wafanyakazi kuichezea na kudanganya,” alisema Rais Samia.

Taarifa ya Ukaguzi Maalumu ya kiuchunguzi ya mfumo wa Enterprise Resource Planning (ERP) unaotumika ndani ya bandari imeonyesha kiasi cha fedha nyingi kimetumika kuajiri makampuni mbalimbali ya kuanzisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato ambayo haikutoa tija.

Uchunguzi huo uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu za Serikali mwezi Juni 2020 na ripoti yake kuwasilishwa mwezi Machi 2021 umebaini kuwa bila kuwa na mpango mkakati wa TEHAMA na bila kushirikisha Mamlaka ya Serikali Mtandao, Bandari iliajiri makampuni kadhaa kuweka mifumo mbalimbali ya ukusanyaji ndani ya bandari.

Kampuni ya Softec Consultant Limited iliajiriwa kwa mkataba Sh milioni 694 kati ya hizo milioni 600 zililipwa kwa kampuni lakini kampuni hiyo haikumaliza kazi iliyopaswa kufanya. Mkataba ukavunjwa.

Iliajiriwa pia 20th century system kwa Dola za Marekani milioni 6.6 ambapo milioni 4.6 zililipwa na mkataba baadae kuvunjwa bila kazi kukamilika. Ikaajiriwa pia SAP East African Limited kwa Dola za Marekani 433,000 lakini pia akaajiriwa mshauri mwelekezi kwa Dola za Marekani 31,920.

“Pesa hizi zote zimeingizwa kwenye mfumo na tunavyo zungumza leo mifumo ile haiko vizuri inachezeleka. Wafanyakazi wanaichezea, wanadanganya na mifumo ambayo haisomani haikusanyi fedha kwa ukamilifu wake,” amesema Rais Samia.

Mbali na malipo hayo, kulikuwa na malipo ya juu kwa wakandarasi hao bila kufuata sheria za manunuzi na matumizi. ripoti ilitaja pia watu waliohusika na uzembe na kupendekeza hatua za kuchukuliwa ambazo hazikuchukuliwa hadi leo.