Wananchi wa Gambia leo wanapiga kura katika uchaguzi wa kihistoria, ambao kwa mara ya kwanza rais wa zamani Yahya Jammeh hayumo kwenye kinyang'anyiro hicho.
Rais wa sasa Adama Barrow aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2016, ana matumaini ya kushinda muhula wa pili katika uchaguzi wa rais unaofanyika leo Jumamosi.
Wagombea sita wanagombea kiti cha urais. Wachambuzi wanasema ushindani mkali ni kati ya wagombea wawili ambao ni Rais Adama Barrow wa chama cha NPP na aliyekuwa Naibu wake Ousainou Darboe anayegombea kwa tiketi ya chama cha United Democratic Party (UDP).
Wagombea wote wamesisitiza juu ya ajenda ya kuleta mabadiliko kwenye kampeni zao wakati ambapo raia wa Gambia bado wanaisaka haki nchini mwao, wanataka uchumi imara baada ya taifa hilo pia kukumbwa na athari zilizosababishwa na janga la corona hali ambayo inachochea idadi kubwa ya watu wanaojaribu kuikimbia nchi hiyo kwa kutumia njia za hatari kwenda barani Ulaya.