Polisi mwenye cheo cha Konstebo, Onesmo Joseph, amekufa baada ya kupigwa risasi na askari mwenzake, aliyetajwa kwa jina la Joseph, walipokuwa wanalinda Benki ya CRDB Tawi la Ruangwa.
Habari za kutoka wilayani humo zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) Mtatiro Kitinkwi, zimeeleza kuwa mauaji hayo yalifanyika juzi saa 6:30 mchana.
Kitinkwi amesema siku ya tukio, askari hao wakiwa lindoni, kulitokea mtafaruku baina yao ndipo Konstebo Joseph akampiga mwenzake risasi sehemu ya nyonga ya mguu wa kulia na kumsababishia maumivu makali.
Alisema chanzo cha ugomvi kilichosababisha askari hao hadi wapigane risasi bado hakijafahamika mara moja lakini baadhi ya watu wanadai walikuwa wanagombea mwanamke, huku wengine, akiwamo Kamanda Kitinkwi, wakidai unatokana na pikipiki.
“Mpaka sasa chanzo cha uhakika kuhusu ugomvi wao bado hakijafahamika licha ya kuwapo taarifa kwamba unatokana na mtuhumiwa kuchelewesha kurejesha pikipiki ya marehemu aliyokuwa ameazima,” alisema Kitinkwi.
Kamanda Kitinkwi alisema Onesmo alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
Aidha, Kitinkwi amesema Konstebo Joseph tayari amefukuzwa kazi na sasa anaandaliwa utaratibu wa kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji linalomkabili dhidi ya mwenzake akiwa raia.