Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Papa Francis ametahadharisha juu ya siasa za kujitafutia umaarufu na ubabe ambazo amesema zinatishia demokrasia ya nchi za Ulaya. 

Papa Francis ametoa wito kwa viongozi kuwa na ari mpya ya kujenga uhusiano mwema badala ya kuzingatia maslahi binafsiya kitaifa. Katika ziara yake nchini Ugiriki, ambayo ni chimbuko la demokrasia, Papa Francis aliwahutubia viongozi wa kisiasa na kitamaduni nchini humo ambapo aliwaonya viongozi wa bara zima la Ulaya juu yya hatari inayolikabili bara hilo. 

Papa Francis amesema umoja na kuwa imara ndio mambo pekee yatakayoweza kutatua masuala muhimu kuanzia kulinda mazingira, kupambana na janga la corona na pia kuutokomeza umaskini. 

Ingawa hakutaja nchi au viongozi maalum, Umoja wa Ulaya hata hivyo uko kwenye mgogoro na wanachama wake Poland na Hungary juu ya masuala ya utawala wa sheria, huku Warsaw ikisisitiza kuwa sheria za Poland zinachukua kipaumbele juu ya sera na kanuni za Umoja huo.