Mamlaka hiyo ilitangaza jana kuwa kuanzi leo mpaka Jumatatu kuna uwezekano mkubwa wa kuwapo kwa mvua kubwa ambayo inaweza ikaleta madhara kwa wananchi wa maeneo hayo.

Mikoa iliyotajwa kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata mvua hizo ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani (kikiwamo kisiwa cha Mafia), Zanzibar, Morogoro na Lindi.

"Uwezekano wa kutokea mvua hizo ni mkubwa lakini athari zake tunategemea kuwa za wastani kwa maeneo mengi yaliyotajwa," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

TMA imetaja athari zinazoweza kutokea kuwa ni maeneo ya makazi kuzungukwa na maji, kusimama kwa baadhi ya shughuri za kiuchumi na kijamii pamoja na ucheleweshwaji wa usafiri.

Mamlaka imewataka wananchi na sekta husika kuchukua tahadhari na kuzingatia utabiri huo walioutoa jana.
Tayari mvua ya msimu imeanza kunyesha maeneo mbalimbali ya nchi na baadhi ya mikoa imeripotiwa mvua hiyo kuleta mdhara kwa jamii.

Mkoani Ruvuma katika Wilaya ya Namtumbo juzi kuliripotiwa nyumba 133 za kijiji cha Likuyesekamaganga kuezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo na kusababisha familia hizo kukosa makazi.