Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amewataka watumishi wa umma kutumia sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara kuendeleza amani na mshikamano mahala pa kazi.

Ametoa wito huo leo (08.12.2021) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru ambapo amewapongeza kwa kazi nzuri iliyochangia maendeleo ya taifa.

" Nimekuja hapa kuwapongeza watumishi wote wa Manispaa kwa niaba ya watumishi wengine wa umma wa mkoa wa Rukwa kwa kazi nzuri mliyofanya hata leo Taifa letu linafikia mafanikio ya miaka 60 ya kuwa huru. Endeleeni kuwa wazalendo kwa taifa letu " alisema Mkirikiti.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya Sebastian Waryuba na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Jacob Mtalitinya watumishi wametakiwa kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia haki,upendo na mshikamano .

Mkirikiti alitumia fursa hiyo kuwataka watumishi hao kuongeza jitihada ili manispaa ya Sumbawanga iwe na maendeleo ikiwemo mapato ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Alikemea pia tabia ya ubinafsi miongoni wa viongozi ndani ya manispaa hiyo hatua inayopelekea kuwepo malalamiko mengi ya watumishi kutopata haki zao na mlundikano wa madeni .

" Nataka Idara ya Utumishi ilipe madeni ya watumishi. Tafuteni fedha kwa kukusanya mapato kwa vyanzo vyenu vyote ili watumishi na wazabuni wanaodai walipwe kwa haraka. Halmashauri yenu sasa haina afya kiuchumi. Badilikeni " alisema Mkirikiti.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka watumishi wote wa serikali mkoani humo kuanza siku ya kwanza baada ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara hapo kesho kwa kubadilika kiutendaji ili wananchi waweze kunifaika kwa kupata huduma bora zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba alisema Mkurugenzi wa halmashauri hiyo anapaswa kubadilika na kuwa karibu na watumishi kwa kutanguliza utatuzi wa kero zao ili shughuli za kuleta maendeleo zisikwame.

" Mkurugenzi umesikia aliyosema Mkuu wa Mkoa, weka muunganiko kati ya watumishi na wakuu wa idara wako . Umoja na mshikamano ukiwepo tutaongeza kasi ya manispaa kustawi " alisema Waryuba.

Mkoa wa Rukwa leo unaadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara Kimkoa  katika sherehe zitakazofanyika kijiji cha Kaengesa wilaya ya Sumbawanga.