Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imetupilia mbali ombi la kutoa hati ya kukamatwa shahidi wa 10 wa Jamhuri, Francis Mroso baada ya ombi hilo kutokidhi matakwa ya kisheria.

Desemba Mosi, 2021 Wakili wa utetezi Fridolin Bwemelo aliomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwa shahidi huyo akidai alitoa rushwa ya Sh90 milioni.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda anayesikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, Wakili Bwemelo aliiomba mahakama itoe amri ya kukamatwa kwa shahidi huyo kaani alikiri kutoa rushwa hiyo.

Akitoa uamuzi huo mdogo, Desemba 6, 2021  Hakimu huyo alisema mahakama inatupilia mbali ombi hilo kwani halijakidhi matakwa ya Sheria inayoruhusu mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa shahidi huyo.

Alisema kifungu namba 52(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kinamlinda shahidi anapotoa ushahidi akiwa chini ya kiapo.

"Ombi la Wakili wa utetezi halijakidhi matakwa ya Sheria inayoruhusu mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa shahidi na mahakama imetupilia mbali maombi na inaona iendelee kusikiliza shahidi anayefuata,"alisema

"Kifungu cha 52(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,kinamlinda shahidi anapotoa ushahidi wake mahakamani akiwa chini ya kiapo,"