Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imetoa rai kwa walimu nchini kuzingatia maadili katika utumishi wao kwani kazi ya ualimu bila maadili haijakamilika.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Willy Komba ameyasema hayo jana jijini Dodoma alipozungumza na Waandishi wa Habari juu ya maadili ya kazi ya Ualimu.

Prof. Komba amesema kuwa elimu kwa ujumla wake imejikita katika maadili hivyo, bila maadili hakuna elimu kwani inawezekana kwenda shule hadi elimu ya juu lakini kama mtu hana maadili atakuwa amesoma lakini hajaelimika.

“Elimu inaenda sambamba na maadili, tunachoona kinachoendelea madarasani, Walimu wetu wengi wanajikita zaidi katika kutoa maarifa kulingana na somo analofundisha lakini suala la maadili wamewaachia viongozi na walimu wenye vipindi vya dini, hii sio sawa kwani kazi ya ualimu ikiweka maadili pembeni inakuwa haijakamilika”, alisema Prof. Komba.

Prof. Komba amefafanua makosa mazito yaliyokithiri kwa Walimu ikiwemo utoro, kugushi vyeti, uhusiano wa kimapenzi, ukaidi na ulevi ambapo kati ya mwaka 2020 hadi 2021, jumla ya makosa ya walimu yalikuwa 1,795 ambapo kwa mwezi Julai hadi Septemba, 2021 makosa ya walimu yalikuwa 184.

Amesisitiza kuwa, adhabu zote zinazotolewa kwa Walimu zinaendana na Kanuni na Tararibu za Tume na kwamba Tume hiyo inajitahidi kutenda haki hivyo, kwa wale ambao hawaridhiki na maamuzi wanaruhusiwa kukata rufaa kwa Kamati ya Nidhamu ya Wilaya, Tume pamoja na kukata rufaa kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Prof. Komba amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuwapandisha madaraja walimu 126,346 pamoja na kurekebisha mishahara yao kwa wakati.

Vile vile amewashukuru Walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutoa elimu na kusimamia miradi mbalimbali ya sekta ya elimu kwani pamoja na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo bado viwango vya ufaulu vinaongezeka.