Kamishna Mkuu TRA Awapongeza Wanamichezo Kwa Kuibuka Washindi Shimmuta
Na Mwandishi wetu
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania amewapongeza watumishi wa Mamlaka hiyo ambao ni wanamichezo kwa kuibuka washindi katika michuano ya SHIMMUTA iliyokuwa ikitimua vumbi hivi karibuni Mkoani Morogoro kwa kutwaa vikombe vitano vya ushindi katika michezo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya wanamichezo hao Bw. Kidata alisema kuwa, juhudi ambazo wamezifanya watumishi hao ni kielelezo cha kuwa na nidhamu na ushirikiano siyo tu katika majukumu yao ya kikazi bali hata baina yao wenyewe.
“Ushindi huu mliouleta unaonyesha dhahiri kwamba mnazingatia maadili ya msingi yanayotuongoza ambayo ni Weledi, Uwajibikaji na Uadilifu kwa sababu bila mambo haya matatu msingefanikiwa kuja na ushindi huu mkubwa, ninawapongeza sana,
Napenda kuwapa taarifa nzuri wanamichezo wote kwamba, nimetoa maagizo ya kufanya matengenezo ya uwanja wetu wa mazoezi uliopo eneo la Kurasini hapa Dar es Salaam na nimetoa maelekezo kwamba ifikapo Mwezi Juni, 2022 nikabidhiwe uwanja huo ili mpate uwanja mzuri wa kufanyia mazoezi,” alisema Bw. Kidata.
Katika mapokezi hayo Kamishna Mkuu Kidata alikuwa na mgeni wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) Bw. John Musinguzi ambaye aliitembelea TRA kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Kamishna Mkuu wa TRA kuhusu masuala ya ushirikiano wa kimkakati hususani katika suala zima la ukusanyaji mapato ya Serikali.
Pamoja na kuwapongeza wanamichezo hao, Kamishna Mkuu huyo wa URA amesema kwamba, watafanya mazungumzo ili iandaliwe mechi ya kirafiki kati ya TRA na URA kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili na kuongeza mahusiano mema baina ya ofisi zetu mbili.
“Hongereni kwa ushindi ambao mmeupata ila ningependa zaidi watumishi wa TRA wafanye mechi ya kirafiki na watumishi wa URA ili kujenga ushirikiano na kuimarisha afya zetu,” alisema Bw. Musinguzi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Michezo wa TRA, Bw. Zahor Salum amemshukuru Kamishna Mkuu na menejimenti nzima ya TRA kwa kuwaruhusu, kuwaamini na kuwawezesha kushiriki michuano hiyo ya SHIMMUTA ambapo ameongeza kuwa bila kuwezeshwa na uongozi huo wasingeweza kupata ushindi huo mnono.
Mashindano ya SHIMMUTA ya mwaka huu yalianza tarehe 13 Novemba na kuhitimishwa tarehe 27 Novemba, 2021 yakishirikisha taasisi 44 za Serikali ambapo katika mashindano hayo, TRA imeibuka kidedea katika michezo mitano ambayo ni mpira wa miguu, bao, draft – Wanaume, draft – Wanawake pamoja na mchezo wa karata.