Ethiopia yaudhibiti tena mji wa Shewa Robi kutoka mikononi mwa waasi
Serikali ya Ethiopia inasema, wanajeshi wake wamedhibiti mji wa Shewa Robit, ulio umbali wa Kilomita 220 kutoka jiji kuu Addis Ababa, ambao wiki iliyopita waasi wa Tigray walidai kuuchukua.
Msemaji wa serikali Legesse Tulu amesema mji wa Shewa Robit Mezezo, Molale, ni miongoni mwa miji midogo ambayo wanajeshi wamefanikiwa kuidhibiti, baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed, wiki iliyopita kwenda katika mstari wa mbele kupambana na waasi hao.
Aidha, serikali inasema jeshi pia limefanikiwa kudhbiti mji wa kihistoria wa Lalibela, unaotambuliwa na Tume ya Umoja wa Mataifa UNESCO kama urithi wa dunia, ambao awali lilikuwa linadhibitiwa na waasi wa Tigray tangu mwezi Agosti.
Makabiliano yalishika kasi nchini Ethiopia, mwezi mmoja uliopita, baada ya waasi wa Tigray kudai kuchukua miji ya kimkakati ya Dessie na Kombolcha, na kusema wanaelekea jijini Addis Ababa.