Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Wathamini nchini kuepuka udanganyifu maarufu kama Tegesha wakati wa kufanya uthamini wa majengo na mali kwa ajili ya ulipaji fidia katika maeneo mbalimbali.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo tarehe 7 Desemba 2021 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka wa Wathamini uliofanyika mkoani Dodoma.

Alisema, ni vizuri Wathamini wakati wa kazi zao wakawa makini na kuhakikisha wanaepuka udanganyifu wa aina yoyote ukiwemo ule wa Tegesha alioueleza kuwa  ulijitokeza sana katika  uthamini uliofanyika Mgodi wa North Mara-Nyamongo.

⁰"Kuweni makini wakati wote mnapokuwa uwandani na kuepuka udanganyifu kama uliofanyika North Mara-Nyamongo, mmea unapandwa usiku na unafanyiwa uthamini na kusababisha serikali kupoteza fedha na mchezo huu umefanyika sana, wote mnajua yaliyotokea tusingependa kama Wizara yajirudie " alisema Dkt Mabula.

Aliwaasa watumishi wote wa sekta ya ardhi na fedha wanaofanya kazi na Wathamini kuwa waaminifu ili wasiwashawishi wathamini kujiingiza kufanya kazi zisizozingatia uadilifu, sheria, kanuni na taratibu na kueleza kuwa ukiukwaji maadili unaleta sintofahamu ama kusababisha malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wateja.

Hata hivyo, Dkt Mabula aliitaka bodi ya Usajili Wathamini nchini kupunguza vikwazo vya usajili ambapo aliitaka kuharakisha zoezi la usajili kwa wale wote waliotimiza vigezo na kueleza kuwa, ucheleweshaji wowote unaofanyika unawakosesha haki katika utumishi ikiwa ni pamoja na kipanda vyeo.

Kwa sasa zaidi ya Wathamini 200 waliopewa mafunzo ya uthamini wanafanya mitihani ya usajili ya Bodi kwa ngazi mbalimbali ambapo baadhi yao wanakamilisha makala za utafiti ili kupata usajili kamili wakiwemo Wathamini wa Ofisi za Mikoa na Halmashauri.

Kupitia mkutano huo Mkuu wa Pili wa Wathamini, Naibu Waziri Dkt Mabula aliitaka Bodi ya Wathamini kusimamia kwa karibu makampuni yote ya uthamini ili yafanye kazi kwa weledi huku akisisitiza zile kesi zinazopelekwa kwenye bodi hiyo na Wizara kutolewa ufumbuzi mapema.

Akigusia kiasi cha fedha shilingi bilioni 50 zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kwa ajili ya mradi wa Kupanga, Kipima na Kumilikisha (KKK) katika halmashauri mbalimbali nchini Dkt Mabula aliwataka Wathamini kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kuzingatia maadili wakati wote wa kutekeleza mradi huo katika halmashauri.

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Wathamini nchini Joseph Shewiyo alimuahidi Naibu Waziri Dkt Mabula kuwa, Bodi yake itahakikisha inasimamia maadili kwa Wathamini pamoja na kusimamia makampuni yote ya uthamini ili yafanye kazi kwa weledi.

“Mhe Naibu Waziri Bodi inaahidi kuyafanyia kazi mambo yote uliyotuagiza ikiwemo kusimamia maadili kwa Wathamini pamoja na kuhakikisha Makampuni ya Uthamini yanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na weledi” alisema Shewiyo.