Na Amiri Kilagalila,Njombe
ALIYEKUWA dereva wa basi la Sharon  lililosababisha ajali na  kusababisha vifo vya askari wanne wa Jeshi la Polisi mkoani Njombe na majeruhi saba, William Emmanuel (28)ahukukumiwa kifungo cha miaka minne jela na kufungiwa leseni yake kwa muda wa miaka miwili.

Akisoma hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Njombe Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Liad Shamshama akiwa na Wakili wa Serikali Andrew Mandwa amesema tukio hilo la ajali lilitokea Februari 2020 maeneo ya mlima wa polisi barabara kuu ya Njombe Songea  saa 12 alfajiri.

Amesema siku ya tukio dereva huyo alikuwa akiendesha basi aina ya Youtong hivyo alipofika maeneo ya mlima wa polisi alilipita  gari lingine sehemu ambayo haikutakiwa kufanya hivyo.Akiwa kwenye mwendo mkali dereva huyo aliligonga gari la polisi aina ya Land cruiser na kusababisha vifo vya askari hao.

"Pamoja na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka minne gerezani mshtakiwa pia amefungiwa leseni yake kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia leo,"amesema Shamshama.Askari waliofariki kutokana na ajali hiyo ni Marianus Hamis Saidi,Heri Athumani Soka, Michael Ernest Mwandu na Dickson Kagoda Maijo.