Na Mwandishi wetu, Dar
Serikali ya Jamhuri ya watu wa China imetoa msaada wa shilingi milioni 714/- kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo msaada huo utakaotumika kuijengea uwezo Wizara ya Mambo ya Nje.

Msaada huo umekabidhiwa Wizarani na Balozi wa China nchini Mhe. Chen Mingjian na kupokelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine jana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kukabidhi msaada huo, Mhe. Mingjian pamoja na Balozi Sokoine wamesaini Mkataba wa Makubaliano kati ya China na Tanzania kuhusu msaada huo pamoja na Hati ya Makabidhiano ya msaada huo.

Msaada huo unafuatia ahadi iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi alipofanya ziara ya kikazi hapa nchini tarehe 7 na 8 Januari 2021.