Polisi ya Ujerumani imesema bomu linaloaminika kuwepo tangu wakati wa vita vya pili vya dunia limelipuka katika eneo la ujenzi karibu na njia ya reli iliyo na shughuli nyingi mjini Munich, na kuwajeruhi watu watatu mmoja akiwa katika hali mbaya.
Moshi mkubwa ulionekana katika eneo la tukio karibu na kituo cha Donners-berger-bruecke. Eneo hilo liko karibu na kituo cha usafiri cha Munich kilichoko kilomita moja kuelekea upande wa Mashariki mwa Ujerumani.
Usafiri wa treni kutoka na kuingia katika kituo hicho umesimamishwa. Mabomu ambayo hayajalipuka hupatikana mara kwa mara Ujerumani miaka 76 baada ya kumalizika kwa vita vya pili vya dunia na mara nyingi hutokea wakati wa shughuli nyingi katika maeneo ya ujenzi.
Kwa kawaida hudhibitiwa na kulipuliwa kwa tahadhari kubwa katika hatua inayohusisha kuwahamishia watu kwa muda katika maeneo salama.