Austria imeondoa vizuizi kwa watu waliopata chanjo kote nchini humo, wiki tatu baada ya kutangaza upya masharti makali ya kupambana na kupanda kwa wimbi la maambukizi ya virusi vya corona.
Masharti hayo, ambayo yanatofautiana na kila jimbo nchini humo, kwa kiasi kikubwa yanaruhusu kufunguliwa tena kwa kumbi za sinema, majumba ya makumbusho na maeneo mengine ya utamaduni na burudani. Maduka yatafunguliwa kesho.
Watu ambao hawajachanjwa wataendelea kuwekewa vizuizi na watabakia majumbani isipokuwa tu kama ni sababu za msingi kama kwenda kununua chakula, kumuona daktari au kufanya mazoezi.
Nchini Ujerumani waandamanaji wamekabiliana na polisi dhidi ya vizuizi vya corona katika miji kadhaa. Kulikuwa pia na maandamano kama hayo katika miji ya Instabul na Ankara nchini Uturuki.