Ikulu ya Afrika Kusini imetangaza kuwa Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na mpigania haki nchini Afrika Kusini, Askofu Desmond Tutu amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90.

Baada ya kifo cha Tutu, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema Tutu alikuwa kiongozi mashuhuri wa kiroho, mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi na mwanaharakati wa kimataifa wa haki za binadamu.

Pia amemtaja kuwa mzalendo ambaye alitoa maana ya ufahamu wa Biblia kwamba imani bila matendo imekufa.

 "Mtu mwenye akili ya ajabu, mwadilifu na asiyeweza kushindwa dhidi ya nguvu za ubaguzi wa rangi, pia alikuwa mpole na mwenye huruma hasa kwa ambao walikuwa wamepitia  dhuluma na vurugu chini ya ubaguzi wa rangi na watu waliokandamizwa  kote ulimwenguni," amesema.

Tutu alikuwa  mmoja wa kati ya watu waliochochea  harakati za kukomesha sera ya ubaguzi wa rangi  iliyotekelezwa na Serikali ya wazungu wachache dhidi ya weusi walio wengi nchini Afrika Kusini kuanzia 1948 hadi 1991.

 Alitunukiwa tuzo ya Nobel mwaka 1984 kwa jukumu lake katika mapambano ya kukomesha mfumo wa ubaguzi wa rangi.