Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekitaka kiwanda cha kuzalisha nyavu za kuvulia dagaa cha Ziwa Net kuzalisha nyavu hizo kwa kuzingatia ubora.

Naibu Waziri Ulega ameyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kuona namna uzalishaji wa nyavu hizo unavyokwenda ambapo uongozi wa kiwanda hicho umetakiwa kuzingatia ubora katika uzalishaji wa nyavu lakini pia kuhakikisha wanazalisha nyavu za kutosha ili wavuvi wasipate shida kuzitafuta.

Kwa upande mwingine Naibu Waziri Ulega amempongeza mwekezaji huyo wa Kiwanda cha Ziwa Net kwa uamuzi wake wa kujenga kiwanda hicho lakini pia kwa kutoa ajira nyingi kwa wanawake ambapo kati ya waajiriwa 18 wanaweke ni 15. Vilevile amewasihi kuhakikisha wanazingatia misingi ya ajira na kuhakikisha hakuna unyanyasaji wa watumishi. Lakini pia amewashauri kuendelea kuwekeza katika utengenezaji wa nyavu za aina nyingine zikiwemo za kuvulia samaki pamoja na nyavu maalum za kutengenezea vizimba vya samaki.

Vilevile amewasihi uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha wanajitangaza lakini pia kuwaalika wadau kuja kuona namna nyavu zinavyozalishwa ili pia waweze kutoa maoni yao kuhusu nyavu hizo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali amesema uwepo wa kiwanda hicho ni muhimu sana kwa wavuvi kwa kuwa itawarahisishia upatikanaji wa nyavu kwa bei nafuu. Lakini pia itapunguza uvuvi haramu kwa kuwa wavuvi watakuwa wakitumia nyavu sahihi.

Meneja Masoko wa kiwanda cha Ziwa Net, Bi. Christina Melkior amesema lengo la kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni kurahisisha upatikanaji wa nyavu za dagaa kwa wavuvi, kukuza na kutangaza zana bora za uvuvi pamoja na kufungua fursa ya ajira kwa vijana watakao ajiriwa katika kiwanda hicho. Pia amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha vipande 66 vyenye urefu wa mita 75 na upana wa mita 3.2 kwa siku ambapo uzalishaji kwa mwezi ni vipande 2000.

Naibu Waziri Ulega pia ametembelea mwalo wa Ihale kukagua maendeleo ya ujenzi wa mwalo huo na kuzungumza na wavuvi, Kituo cha kupumzisha Mifugo cha Lamadi wilayani Busega mkoa wa Simiyu na kiwanda cha kuchakata mabondo cha Pesca Perch wilayani Magu mkoa wa Mwanza.