Idadi ya watu wanaokufa kutokana na matumizi ya mihadarati imevuka laki moja kwa mwaka nchini Marekani.

Wataalamu nchini humo wamesema vifo hiyvo vimetokana na matumizi zaidi ya mhadarati unaoitwa Fentanyl. 

Idara kuu ya kudhibiti magonjwa ya Marekani CDC imetoa taarifa hiyo na kueleza kwamba watu wengi zaidi wanakufa kwa mwaka kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya kuliko wale wanaokufa kutokana na kupigwa risasi au na ajali za barabarani. 

Idara hiyo imesema matumizi ya mihadarati yameongezeka kwa asilimia 28.5 kati ya mwezi Mei mwaka 2020 hadi mwezi Aprili mwaka huu wa 2021. 

Mkurugenzi wa Kitaifa wa Kudhibiti sera ya Dawa za Kulevya nchini Marekani Dr. Rahul Gupta amesema hali hii isiyo ya kawaida haikubaliki na inahitaji kutafutatiwa majibu ya haraka.