Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
WAZIRI ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amewapiga marufuku wakurugenzi wa Halmashauri kuacha tabia ya kutoa adhabu ya kuwashusha vyeo walimu wakuu Pamoja na maafisa elimu kata kwa kisingizio shule zao hazijafaulisha .


Ameeleza,adhabu hizo zinasababisha ongezeko la udanganyifu wa mitihani mashuleni na kuvunja moyo walimu na maafisa hao.


Ummy aliyasema hayo katika mahafali ya 29 ya chuo Cha Wakala wa maendeleo ya elimu (ADEM ) Bagamoyo,Pwani kwa wahitimu wa stashahada ya uongozi na usimamizi wa elimu-DEMA,stashahada ya ukaguzi wa shule na astashahada ya uongozi, usimamizi na utawala katika elimu.


Alielezea,kabla ya kuwapa adhabu na kuwashusha vyeo vyao Ni vyema kukafanywa tafiti za kina kujua sababu zilizosababisha shule hizo kufanya vibaya kitaaluma.


Aidha Ummy alipiga marufuku watoto kusomeshwa muda wa ziada nyakati za usiku na kushindwa kupata muda wa kupumzika huku akitoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia shule za Sekondari za Serikali kuwapa likizo wanafunzi wote mwezi Desemba .


“Watoto wanapaswa wapumzike , haiwezekani mtoto kusoma shule na akirudi darasani usiku akeshe saa 2-9 alfajiri anasoma huko Ni kumuumiza mtoto ,


“Dakika 120 kusoma mtoto zinamtosha ,na hapa niwaombe wazazi na walezi tusitake watoto wetu wahenyeshwe ndio tujue wanasoma Sana ama shule ndio zinasomesha Sana “alisema Ummy.


Mtendaji mkuu ADEM Dkt.Siston Mgullah alielezaWakala Una majukumu ya kuendesha mafunzo ya uongozi na utawala katika elimu,kuandika na kusambaza makala mbalimbali na kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalum kuhusu uongozi na utawala katika elimu ili kuzishauri wizara zinazosimamia elimu juu ya namna bora ya kuendesha Taasisi za elimu nchini.


Mgullah alifafanua,katika kutekeleza majukumu hayo,ADEM inaendesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika uongozi, usimamizi wa elimu na uthibiti ubora wa shule.


Wahitimu wa mafunzo hayo Ni 1,082 kutokea kampas ya Bagamoyo,Mwanza na Mbeya.