Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amezitaka bodi za wakurugenzi za TAFIRI, TAFICO na FETA kuhakikisha uchumi wa bluu unakuwa katika mikono na mifuko ya wananchi.

Akizungumza (02.11.2021) jijini Dodoma wakati akizindua rasmi bodi za wakurugenzi za Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA), Mhe. Ndaki amesema taasisi hizo ambazo ziko chini ya wizara yake zinapaswa kuhakikisha uchumi wa bluu ambao serikali inataka kuhakikisha inavua samaki katika bahari kuu unakuwa na manufaa kwa wananchi.

Mhe. Ndaki ameziambia bodi hizo kuhakikisha zinatoa ushauri wa kina kwa menejimenti na kufanya kazi kwa ufanisi kwa kufungua kurasa mpya na kusimamia vyema majukumu ya taasisi hizo ili zifanye kazi na kufikia malengo yenye tija.

“Tunataka uchumi wa bluu uonekane kwenye mikono ya watanzania lakini pia katika mifuko ya watanzania.” Amesema Mhe. Ndaki

Aidha, amezitaka bodi hizo kutunga sheria, sera na kanuni na kuhakikisha zenye kasoro zifanyiwe maboresho ili kuhakikisha zinaboresha huduma kwa wananchi, kwa kuwa lengo la serikali ni kutaka wananchi kuchangia vya kutosha kwenye pato la taifa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amezitaka bodi za wakurugenzi za TAFIRI, TAFICO na FETA kuhakikisha zinaifanya sekta ya uvuvi kufanya kazi kibiashara pamoja na kufanya tafiti ya matatizo ya kawaida ya wavuvi ili kuyapatia majawabu.

Pia amesema ana imani taasisi hizo zinaweza kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha zinazalisha ajira kupitia sekta ya uvuvi ili wananchi wengi waingie katika ajira kupitia sekta hiyo.

Ameongeza pia wajumbe wanapaswa kufikia malengo ya aliyewateua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyewateua wenyeviti wa bodi pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki aliyewateua wajumbe wa bodi.

Mhe. Ulega amezitaka taasisi hizo kufanya vizuri kwa kumsaidia Rais Samia kuweza kufikia malengo ya sekta ya uvuvi kuwa na tija zaidi kwa taifa.

Awali akizungumza katika uzinduzi wa bodi za wakurugenzi za TAFIRI, TAFICO na FETA, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema ana uhakika wajumbe watafanya kazi kwa kushirikiana na menejimenti ya taasisi hizo ili ziweze kupata maendeleo mazuri wakati wa uongozi wa bodi hizo.

Pia amesema ili wajumbe waweze kuelewa kwa upana juu ya majukumu ya wizara, amesema ni wajibu wajumbe hao wafahamu majukumu mbalimbali yakiwemo ya kusimamia sera na mipango ya rasilimali ya uvuvi, kusimamia pamoja na kufanya tafiti katika maeneo ya uvuvi.

Akizunguma kwa niaba ya wenyeviti wa bodi za wakurugenzi za TAFICO na FETA, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TAFIRI Alhaj Yahya Mgawe amesema watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi zaidi ili sekta ya uvuvi ifikie malengo yaliyotarajiwa na serikali na hatimaye kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa 

Amesema wamepewa heshima kubwa ya kuzisimamia taasisi hizo na kwamba watahakikisha wanasimamia vyema dira na malengo yaliyowekwa kwa kila taasisi.

Bodi za wakurugenzi za Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA), zilizozinduliwa rasmi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Masimba Ndaki zitasimamia taasisi hizo kwa kipindi cha miaka mitatu, ambapo mwenyekiti wa bodi ya TAFIRI ni Alhaji Yahya Mgawe, mwenyekiti bodi ya TAFICO Prof. Yunus Mgaya na mwenyekiti bodi ya FETA ni Dkt. Blandina Lugendo.

Mwisho.