Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekutana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) nchini Tanzania Veeraya Kate Somvongsiri na kumuelezea hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha sekta ya ardhi nchini.

Bi Kate alimtembelea Waziri Lukuvi katika Ofisi za Wizara zilizopo eneo la Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma  tarehe 11 Novemba 2021 kwa lengo la kujitambulisha.

Katika mazungumzo yao, Waziri Ardhi alimueleza Mkurugenzi huyo wa USAID nchini kuwa, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iko katika jitihada mbalimbali kuhakikisha ardhi yote ya Tanzania inapangwa na kupimwa.

Kwa mujibu wa Lukuvi, pamoja na juhudi hizo, Wizara yake imeanza pia kuhifadhi kumbukumbu za ardhi kwa kutumia mfumo wa kidigitali na kuachana na ile mifumo ya zamani iliyokuwa ikitumia karatasi nyingi huku ikianza kutoa hati za ardhi za kielektroniki yenye kurasa moja.

‘’Tunataka kwenda mbele zaidi katika teknolojia ya uhifadhi wa kumbukumbu zetu za ardhi na tumeanza kuscan taarifa zetu za ardhi katika teknolojia na tumeanza pia kutoa hati za kielektroniki kwenye mkoa wa Dar es salaam na Dodoma’’ alisema Lukuvi.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema, pamoja juhudi za Wizara kuhakikisha ardhi inapimwa vipaumbele pia vimeelekezwa kwenye maeneo ya vijijini ikiwemo kutumia njia rahisi ya upimaji na kutoa hati za kimila ili kulinda maeneo pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

‘’Kwa sasa wizara ya ardhi inafanya jitihada kubwa kuhakikisha ardhi inapangwa na kupimwa ili kuepuka migogoro ya ardhi na wakati huo kuwawezesha wananchi kiuchumi pamoja na kuiwezesha serikali kupata mapato.’’ Alisema Mary

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani USAID Veeraya Kate Somvongsiri aliunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kupitia Wizara ya Ardhi na kusema kuwa Shirika hilo liko tayari kushirikiana na wizara ya ardhi kusaidia sekta ya ardhi nchini.

‘’Nimetembelea mkoa wa Iringa kunakofanyika mradi wa upimaji ardhi wa teknolojia rahisi vijijini (Feed the Future Tanzania Land Tenure Assistance) na kuona jinsi mradi huo ulivyofanikiwa ambapo niliangalia namna bora ya kusaidia miradi kama hiyo na nimeomba kupatiwa proposal kuhusiana na mafanikio ya mradi’’.alisema Kate

Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo la Marekani USAID imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali nchini Tanzania katika nyanja za nishati, uhifadhi wa mazingira, huduma za afya ya uzazi na afya ya mtoto, huduma za kubabiliana na malaria na msaada kwa wakimbizi.