Lydia Churi- Mahakama, Lushoto
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ametaja mafanikio makubwa sita ambayo Tanzania imeyapata katika kipindi cha miaka 60 tangu uhuru wake Desemba 9, 1961.

Akizungumza katika mahafali ya 21 ya chuo cha uongozi wa Mahakama Lushoto ambapo alikuwa mgeni rasmi, Prof. Kabudi amesema Tanzania inaadhimisha miaka 60 ya uhuru ikiwa ni taifa imara na siyo mkusanyiko wa makabila yasiyokuwa na umoja.

Alisema kuwa ndani ya miaka 60 ya uhuru Tanzania imeingia katika uchumi wa kati.  Alifafanua kuwa wakati wa uhuru, Tanganyika ilikuwa nchi maskini kuliko zote Afrika ya Mashariki na Kati, lakini leo ni nchi ya pili kwenye ukanda huo kuingia uchumi wa kati miaka mitano kabla ya wakati uliokuwa umetarajiwa, tena pamoja na kuwepo kwa ugonjwa wa UVIKO 19 uliosababisha uchumi kuporomoka kwenye mataifa mengi duniani.

“Tunasherehekea miaka 60 ya uhuru tukiwa ni taifa lililojikita katika kuenzi na kudumisha tunu za taifa ambazo ni amani, umoja, mshikamano, utu, haki, heshima, uhuru na demokrasia”, alisema Prof. Kabudi.

Alisema mafanikio mengine makubwa ambayo nchi imeyapata katika kipindi cha miaka 60 ni kuwa taifa lenye udhubutu na moyo wa kujitegemea katika kufanya mambo makubwa kwa rasilimali zake yenyewe.  Alisema, hivi sasa Tanzania inatekeleza miradi mikubwa Ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere litakalozalisha umeme wa Megawatt 2,115 pamoja na kujenga reli ya kisasa ya umeme ambayo kwa mujibu wa wataalamu itachukua miaka 150 kabla ya  kufanyiwa ukarabati mkubwa. Miradi yote hii na mingine inatekelezwa kwa fedha za ndani.

Waziri wa Katiba na Sheria alisema, Tanzania inasherehekea miaka 60 ya uhuru ikiwa imetangaza kwamba mali asili zote na rasilimali zote ni mali ya watanzania. Alisema hatua hii imewezesha kurejewa upya kwa mikataba na kampuni kubwa zikiwemo za madini ili wananchi wafaidike na mali zao. “Nathubutu kusema kuwa katika nchi za Afrika sisi ni wa kwanza kufanya hivyo”, alisisitiza.

Prof. Kabudi alisema Tanzania imeidhihirishia Dunia ukomavu wa kisiasa na umadhubuti wake katika ukatiba (Constitutionalism). Alisema nchi ilionesha ukomavu mkubwa wa kiasiasa na utaratibu wake wa kisiasa na kikatiba katika kipindi cha mpito kwa amani na utulivu baada ya kifo cha Rais wa awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli, na kwa mujibu wa katiba, Makamu wa Rais aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwaasa wahitimu 575 wa fani ya Sheria, Prof. Kabudi amewataka kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza mazuri yaliyoanzishwa. “Mkiwa ni vijana wa taifa hili, kazi yenu ni kuyaendeleza hayo yote”, alisisitiza.