Na.Erick Mungele,Dodoma
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji, amewataka wakuu wa Mikoa nchini kuweka jitihada za pamoja ili kurahisisha utekelezaji na usimamizi wa Mfumo huo katika ngazi ya mikoa na halmashauri zote nchini.

Kauli hiyo ameitoa  November 13,2021 jijini Dodoma wakati wa semina ya kujenga uelewa wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi iliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Dkt. Ashatu, amesema kuwa wakuu wa mikoa ndio wasimamizi  wa shughuli zote na vipaumbele vya Serikali katika Mikoa yao hivyo wana jukumu kubwa la kuwahamasisha wananchi na wadau katika utekelezaji na matumizi ya mfumo huo na kuhakikisha ifikapo mwezi Aprili, 2022 asilimia 75 ya watanzania wawe na Anwani za Makazi na Postikodi katika maeneo yao .

“Natoa wito wakuu wa mikoa wote kuweka jitihada za pamoja katika uhamasishaji wanachi katika uwekezaji wa mfumo wa anuani za makzi na posta ili kila mwananchi aweze kufikiwa na huduma ifikapo mwaka 2024”amesema Dk.Ashatu

Aidha Dk.Ashatu amesema kuwa Wakuu wa Mikoa wana jukumu la kuzielekeza halmashauri kukamilisha utayarishaji na uidhinishaji wa majina ya barabara na mitaa na kutengeneza sheria ndogo za utekelezaji na matumizi ya mfumo wa Anwani na Makazi na Postikodi katika ngazi ya halmashauri

Hata hivyo Dkt. Ashatu ameishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa utayari, ushirikiano mkubwa na ushauri kwa Wizara ya kisekta kutenga bajeti ya sekretarieti ya mikoa ili kuweza kufanikisha malengo ya Serikali ya kila mwananchi kuwa na Anwani za Makazi.

Kwa upande wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa mbali na vipaumbele vingi walivyonavyo katika Wizara hiyo Mfumo wa Anwani na Makazi ni muhimu hasa katika kuimarisha huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi

Amesema kuwa kupitia utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi Idara ya Uendelezaji Miji itahakikisha miji inapimwa na kupangwa vyema ili kurahisisha ufikishaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa jamii.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe.John Mongela ,amesema semina hiyo itawasaidia kuwapa uelewa wa pamoja kuhusu mfumo huo wa anuani za makazi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa nchi ya Tanzania inapaswa kuwa mfano katika utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi hasa kwa kuzingatia utekelezaji wa Mfumo huo ni matakwa ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) ambapo Makao Mkuu ya Umoja huo yapo Tanzania na kama nchi ni wajumbe wa Baraza la Utawala na Baraza la Uendeshaji wa Posta Duniani (UPU) wenye jumla ya nchi wanachama 192

Naye Naibu Katibu Mkuu (Elimu) wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Gerald Mweli amesema kuwa sekretarieti za mikoa zina wajibu wa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa  Mfumo wa Anwani za Makazi  katika maeneo yao ya kazi ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 halmashauri zimetenga kiasi cha shilingi milioni 900.1 za utekelezaji wa Mfumo huo ikilinganishwa na kiasi ncha shilingi milioni 553.85 kwa mwaka 2021, milioni 47.2 mwaka 2020, milioni 18.79 mwaka 2019 na milioni 8.12 kwa mwaka 2018 ambayo inaonesha kuwa bajeti ya utekelezaji wa mfumo huo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Terack akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa hao amesema kuwa kazi yao ni kutekeleza maelekezo yote ya Serikali katika maeneo yao na kupitia semina hiyo wamejifunza, wamepokea na kuelewa kuhusu Mfumo huo na kuahidi wanaenda kutekeleza kwa kushirikiana na Wizara ili kwa pamoja wanaenda kuijenga nchi ya Tanzania kwa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na anwani ya Makazi.