Watu watano wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati wa maandamano ya kudai utawala wa kidemokrasia nchini Sudan hapo jana Jumamosi. 

Haya ni kwa mujibu wa kamati kuu ya madaktari nchini Sudan. Kamati hiyo imedai kuwa vikosi vya baraza la mapinduzi ya kijeshi nchini humo, vilivamia hospitali ya Al Arbaeen huko Obdurman na kuwashambulia vikali madaktari waliokuwa kazini, kuwajeruhi raia, familia zao na kuwakamata baadhi yao. 

Hata hivyo polisi imekanusha kutumia risasi dhidi ya waandamanaji na kusema vikosi vya ulinzi vilitumia nguvu ya kawaida. Polisi iliwashutumu waandamanaji hao kwa kushambulia vituo kadhaa vya polisi na kudai kwamba maafisa wake 39 pia walijeruhiwa. 

Ripoti hizo zinakuja baada ya waandamanaji kuingia tena mitaani kujibu mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25 na uamuzi wa upande moja wa kamanda wa jeshi jenerali Abdel Fattah al- Burhan ya kuteuwa baraza kuu jipya la utawala siku ya Alhamisi huku akijitangaza kuwa mwenyekiti wa baraza hilo.