Idadi ya kila siku ya maambukizo mapya ya virusi vya corona nchini Ujerumani imefika kileleni. 

Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza, Robert Koch, imerikodi maambukizi mapya 33,949 ndani ya siku moja. 

Hayo ni maambukizo 172 zaidi ya yaliyorekodiwa mwezi Desemba 2020. Hata hivyo, haijulikani kama idadi hiyo inajumuisha maambukizo yaliyochelewa kuripotiwa baada ya kipindi cha likizo kumalizika. 

Rais wa taasisi ya Robert Koch, Lothar Wieler, ameonya kwamba iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa basi kutazuka wimbi la nne la ugonjwa wa COVID-19. 

Aidha amesema maambukizo yameongezeka kutokana na watu ambao hawakupigwa chanjo na kupuuza kuzingatia sheria. 

Mawaziri wa afya wa majimbo yote ya Ujerumani watakutana leo kujadili jinsi ya kuishughulikia hali hiyo.