Askari wa Jeshi la Polisi Madagascar wenye silaha wamevamia kambi ya timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wakitaka kuwachukua kwa nguvu wachezaji watatu wakidai wana maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).


Wachezaji hao ni Nahodha, Mbwana Samatta, kipa namba moja Aishi Manula pamoja na beki kitasa Bakari Mwamnyeto.

Tukio hilo, limetokea asubuhi ya leo Jumapili, tarehe 14 Novemba 2021, kwa askari hao kuvamia hotel waliofikia Stars na kusababisha taharuki kwa watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hayo yamejiri saa chache zimebaki kabla ya Stars yenye pointi saba kushuka dimbani nchini humo kuvaana na Madagascar kuanzia saa 10:00 jioni kukamilisha mchezo wa kundi J wa kuwania kufuzu kombe la dunia nchini Qatar 2022.