Na Benny Mwaipaja, Arusha
KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba amewataka Wakaguzi Wakuu wa Ndani kuzingatia maadili ya kazi zao kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa wanapotimiza majukumu yao ili kaguzi wanazofanya ziwe na tija kwa taifa.
Bw. Tutuba ametoa rai hiyo Mjini Arusha wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Wakaguzi Wakuu wa Ndani uliowashirikisha wakaguzi 500 kutoka taasisi za umma nchini uliolenga kuweka mkkakati ya namna ya kuboresha tasnia ya ukaguzi nchini.
Alisema kuwa vitendo vya ukikwaji wa maadili vinasababisha thamani ya fedha inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi isionekane.
Aidha, amewaagiza Wakaguzi hao Wakuu wa Ndani kwenda kukagua fedha za kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhini ya Uviko-19 na kutoa taarifa Serikalini kila mwezi.
Katika hatua nyingine, Bw. Tutuba ameiagiza Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Fedha ya Wizara ya Fedha na Mipango kutengeneza moduli ya mfumo wa utekelezaji wa miradi kitaifa itakayotumika kusajili miradi yote inayotekelezwa hapa nchini ili kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema hatua hiyo itawasaidia hata wakaguzi wa ndani kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuwa moduli hiyo itakuwa ikitumika kukusanya taarifa za utekelezaji wa miradi pamoja na picha zinazoonesha maendeleo ya ujenzi wake hatua kwa hatua.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (IAG) Bw. Athumani Mbuttuka, alisema kuwa Mkutano huo umekuwa na manufaa makubwa kwa umetumika kukumbushana wajibu wa utekelezaji wa mjukumu ya Wakaguzi Wakuu wa Ndani.
Alibainisha kuwa Mkutano huo pia umeibua changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya ukaguzi ikiwemo uhaba wa watumishi na vitendea kazi mambo ambayo Serikali imeahidi kuyafanyia kazi.
Akizungumza kwa niaba ya Wakaguzi Wakuu wa Ndani, Bi. Neema Kiure aliipongeza Serikali kwa kuandaa Mkutano huo uliotoa fursa kwa wakaguzi hao kujitafakari namna wanavyotekeleza majukumu yao na kuahidi kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya watendaji hao.
Alibainisha kuwa Wakaguzi Wakuu wa Ndani ni jicho la Serikali katika kuhakikisha kuwa rasilimali fedha na miundombinu mingine inatumika kama ilivyokusudiwa ili kuleta thamani halisi ya uwekezaji huo wa Serikali katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo.
Mkutano huo wa Mwaka wa Wakaguzi Wakuu wa Ndani umefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha.