Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla leo kutoa miezi mitatu kwa Shirikisho la Vyama vya Waendesha Bodaboda Jijini Dar es salaam kuweka mpango kazi kuwapanga vizuri Bodaboda ikiwa ni pamoja na utaratibu rasmi wa kuingia mjini na kutoka, haya ni maazimio ambayo ameafikiana nao kwenye kikao walichoketi leo ambacho kilijumuisha Viongozi wa Bodaboda, Jeshi la Polisi, LATRA, TARURA na TANROADS.

Miongoni mwa maazimio yaliyotolewa na kikao hicho ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Kamati iliyoundwa ni pamoja na shughuli za Bodaboda kufanyika sambamba na kulinda taswira ya Jiji, uwepo wa vituo rasmi vya Bodaboda vinavyotambulika, uvaaji wa sare, kofia ngumu na Bodaboda kuwa sehemu ya kuwafichua Wahalifu ambapo RC Makalla amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia inathamini kazi ya Bodaboda kutokana na shughuli hiyo kutoa ajira kwa idadi kubwa ya Vijana.

Baadhi ya Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya waendesha Bodaboda akiwemo Said Kagomba ambae ndiye Mwenyekiti wa Shirikisho ameishukuru Serikali kwa kukaa meza moja na Shirikisho kuangalia namna bora ya kushughulikia jambo hilo na wameahidi kushirikiana na Serikali kuweka mazingira bora ya biashara hiyo ili Bodaboda wa Dar es salaam wawe mfano wa kuigwa.